Kanuni kupitiwa kukilinda Kiwanda cha Mkulazi

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema watafanya kila jitihada kuhakikisha wanakilinda Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi kitakachozalisha sukari ya viwandani.

Bashe amesema Bodi ya Sukari Tanzania imeanza utaratibu wa kupitia kanuni za namna ya kukilinda kiwanda hicho, kitakachowezesha kupunguza tani 50,000 za sukari za viwanda zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.

Bashe amesema hayo leo Jumatano Agosti 7, 2024 wakati akizungumza katika uzinduzi wa kiwanda hicho, kinachomilikiwa na Uongozi wa Kampuni ya Hodhi ya Mkulazi (MHCL), kilichoanza kujengwa mwaka 2021, wilayani Kilosa mkoani Morogoro.

Uzinduzi wa kiwanda hicho, umefanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye leo anahitimisha ziara yake ya kikazi ya siku sita mkoani Morogoro.

“Niwape moyo watu wa Mkulazi hii bidhaa itaingia sokoni kwa uwezo wa Mungu sio muda mrefu, kabla ya Juni 2025 kanuni itakuwa imebadilishwa ili kukilinda kiwanda hiki kinachozalisha sukari ya viwandani pia,” amesema Bashe.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Seleman Jafo amesema Rais Samia anaendelea kuweka historia ya kuongeza viwanda katika utawala wake hasa katika sekta ya sukari ambayo imekuwa na changamoto kubwa.

“Sasa unakwenda kuweka historia, chini ya sera zake, Kilombero Sugar itazalisha tani 271,000, Kagera tani 155,000, hapa tani 50,000 na Bagamoyo Sugar 35,000. Ndani ya muda mfupi zaidi tunakwenda kukidhi matakwa ya matumizi ya sukari,” amesema Dk Jafo.

Related Posts