Takwimu ugumba, shinikizo la damu zaishtua Serikali

Dar es Salaam. Takwimu za idadi ya wagonjwa waliopimwa na kukutwa na shinikizo la juu la damu na wanawake wanaohitaji usaidizi wa kupata watoto ‘ugumba’ zimeishtua Serikali ya Tanzania.

Takwimu hizo zimeonyesha jumla ya wanawake 3,810 wamejitokeza katika kambi ya madaktari bingwa kwenye hospitali 184 za halmashauri, huku asilimia 34 ya wagonjwa walioonwa walikuwa na shinikizo la juu la damu.

Hayo yamezungumzwa leo Jumatano Agosti 7, 2024 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipokuwa akitoa ripoti ya utoaji wa huduma za kibingwa kwenye hospitali 184 ngazi ya halmashauri kupitia mpango wa madaktari bingwa wa Samia, zilizofanyika Mei mpaka Julai 2024.

Amesema jumla ya wagonjwa 70,000 walioonwa na kambi hiyo na kati yao 22,057 wa magonjwa ya ndani, shinikizo la juu la damu wagonjwa 7,529 sawa na asilimia 34 ikifuatiwa na matatizo ya mfumo wa chakula wagonjwa 4,158 sawa na asilimia 9.

“Shinikizo la juu la damu ni magonjwa yaliyoongoza kwa asilimia 34, hii ni alamu kwetu. Itabidi tufanye uchambuzi up ya kwa maana ripoti ya hivi karibuni ilituonyesha asilimia 25 ya Watanzania, huku imeongezeka, wataalamu wanaingia kuchunguza tutaona tupo asilimia ngapi ikifika Desemba,” amesema Waziri Ummy.

Pamoja na hilo, ametoa agizo kwa kila Mtanzania kuhakikisha anachunguza shinikizo la juu la damu kila anapokwenda kituo cha afya na kuzingatia mtindo bora wa maisha.

Kufuatia hali hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Dk Peter Kisenge ameiambia Mwananchi wagonjwa wanaofuata huduma katika vituo va afya idadi ya wenye shinikizo ni kubwa ikilinganishwa na katika jamii.

“Tunapoenda kwenye jamii tunaomba takwimu kama hizo, kwa JKCI hapa asilimia 30 ya wagonjwa tunaowaona wana shinikizo la juu la damu na kwenye kambi tukiwafuata mitaani tunawapata asilimia 25,” amesema.

Dk Kisenge ambaye pia ni bingwa wa magonjwa ya moyo ameshauri jamii kubadili mtindo wa maisha, akisema asilimia kubwa ya watu hawafanyi mazoezi huku wakiwa na ulaji mbaya, unywaji pombe uliokithiri, uvutaji sigara uliokithiri na kuwa na unene kupita kiasi vitu vinavyochangia tatizo hilo.

Akizungumzia suala la ugumba, Waziri Ummy amesema kati ya wateja 18,044 walioonwa na madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, matatizo ya ugumba yaliongoza.

Amesema wagonjwa 3,810 sawa na asilimia 21 walikutwa na changamoto ya ugumba, kujifungua wateja 2,529 sawa na asilimia 14 na tatizo la kutokwa na damu nyingi ukeni isivyo kawaida wagonjwa 2,108 sawa na asilimia 12.

“Hili nalo tunalitafakari kama tunakutana na wagonjwa wa ugumba wengi tunaliangalia, inabidi tulitafakari zaidi na hii ni changamoto kwa Watanzania wengi ambao wamekuwa wakishindwa kupata matibabu kutokana na gharama kuwa kubwa,” amesema Waziri Ummy.

Alipoulizwa kuhusu mchakato wa upandikizaji mimba katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Benjamin Mkapa, amesema: “Tumeshakamilisha kituo cha upandikizaji mimba nilitaarifiwa kuhusu uzinduzi kwa upande wa Muhimbili ambao tayari wameshaanza kuwahudumia wagonjwa tayari. Kuna mawili matatu ya kukamilisha.

“Changamoto iliyoonekana ni gharama za sekta binafsi zinaleta changamoto na suala hili linawafanya wanawake wengi wanapitia unyanyapaa na ni sehemu ya haki ya mwanamke na mwanamume kupata huduma. Kwa sasa nafanya uchambuzi wa gharama ikiwezekana tuzipunguze kwa asilimia kubwa,” amesema.

Waziri Ummy amesema katika kambi hiyo, hospitali 184 zilizopo katika mikoa 26 zilifikiwa na jumla ya wagonjwa 70,000 walionwa.

“Kati yao, madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani waliona wagonjwa 22,057 sawa na asilimia 32 magonjwa ya wanawake na uzazi 18,044 (26) watoto 14,466  (21) na madaktari bingwa wa upasuaji waliona wagonjwa 10,578 (15) na kwa jumla wateja 4,652 sawa na asilimia 7 walipata huduma za upasuaji,” amesema.

Aidha amesema katika kambi hiyo madaktari bingwa wameimarisha huduma za watoto wachanga katika wodi ‘NCU’ 129 zilizokuwepo, wameanzisha 27 mpya na wamesaidia hospitali 28 kuweka mipango kazi ya kuanzisha huduma hizo ndani ya miezi 6.

Aidha amesema Serikali itaendelea kuziimarisha NCU kwa kuhakikisha zina vifaa tiba vya kutosha, kuimarisha ujuzi wa watoa huduma na kuongeza wodi zingine katika ngazi za vituo vya afya.

Mkurugenzi msaidizi anayesimamia huduma za watoto wachanga, watoto na vijana Wizara ya Afya, Dk Felix Bundala amesema wodi maalumu kwa watoto wachanga ni muhimu katika kutunza watoto wachanga hasa wanaozaliwa na uzito pungufu.

“Yametoka mapendekezo lazima kila halmashauri iwe na wodi hizo, watoto hawa wanahitaji hewa wapate joto, kulishwa na wanazaliwa na uzito pungufu wasipopata huduma ndani ya saa 48 tuna hatari ya kuwapoteza asilimia 70 yao,” amesema Dk Bundala.

Related Posts