Wimbi la joto kali lazusha kizaazaa kila kona ya dunia – DW – 07.08.2024

Watu wa barani Afrika, mataifa ya Kiarabu na eneo la Asia na Pasifiki ndiyo wanakumbwa na hali ya juu zaidi ya joto.Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya mezi Julai iliyotolewa na Shirika la Kazi Duniani, ILO. 

Kuanzia Ufilipino hadi India, na hadi Mali, ukosefu wa takwimu za kuaminika kuhusu vifo vinavyotokana na joto, hudhoofisha juhudi za kupunguza hatari ya joto kali na kutoa ulinzi bora kwa watu walioko hatarini zaidi, kama vile wahamiaji na watu wenye ajira za muda. ILO imesema hali hii husababisha takribani vifo 19,000 kwa mwaka.

Kukusanya takwimu sahihi ili kueleza kuhusu sera ya serikali juu ya kupunguza joto kali ni muhimu zaidi kama ambavyo mabadiliko ya tabianchi yanavyosababisha viwango vya joto duniani na ongezeko la vifo vitokanavyo na joto.

Mwaka uliopita, ulirekodiwa kuwa mwaka wenye joto kali zaidi na Julai 21, mwaka huu wa 2024, ilikuwa siku yenye joto zaidi kuwahi kurekodiwa wakati ambapo joto kali liliyakumba maeneo ya Marekani, Ulaya na Urusi.

Tarik Benmarhnia, mtaalamu wa kufuatilia jinsi mazingira yanavyoathiri afya ya binadamu, katika Chuo Kikuu cha California San Diego, anasema katika muktadha wa mabadiliko ya hali ya hewa, wanashuhudia muda mrefu zaidi wa siku za joto kali ambazo zinadumu kwa muda mrefu usiku, na hivyo watu hawatokuwa na mapumziko. Benmarhnia anasema wataalamu wa afya hawatambui kikamilifu jinsi suala hilo lilivyo kubwa.

Vifo na magonjwa ni miongoni mwa athari za kuongezeka viwango vya joto

Romania | Wimbi la joto kali
Shirika la Kazi duniani ILO linasema viwango vya juu vya joto vinapunguza ufanisi kazini. Picha: DANIEL MIHAILESCU/AFP/Getty Images

Kulingana na takwimu za wizara ya afya nchini Ufilipino, ambako wiki mbili za joto kali mwezi Aprili, zilisababisha shule kufungwa, vifo saba vitokanavyo ya joto na magonjwa 77 yanayohusiana na joto, yaliripotiwa kuanzia mwezi Januari hadi Mei mwaka huu.

Mwanaharakati wa chama cha wafanyakazi, Lucas Ortega anasema takwimu kama hizo haziakisi hatari ya joto kali wanayokumbana nayo wafanyakazi.

Ortega ambaye ni msemaji wa Shirikisho la Wafanyakazi nchini Ufilipino anasema wanajua kuna maelfu ya wafanyakazi katika sekta ya usafirishaji, ujenzi, na viwandani, lakini hawajui ni wangapi kati yao walikabiliwa na joto kali.

Upatikanaji wa takwimu sahihi kuhusu vifo vitokanavyo na joto kali ni mgumu, kwa sababu maafisa wa afya hawahusishi vifo hivyo na joto haswa, bali kwa magonjwa yanayotokana na viwango vya juu vya joto, kama vile matatizo ya mishipa ya moyo na figo. Benmarhnia anasema hilo hulifanya joto kuwa muuaji wa kimya kimya.

Mtafiti Barrak Alahmad, anasema ni nadra sana kukuta vyeti vya vifo vinaeleza moja kwa moja kuwa joto kali ndiyo sababu ya kifo. Kulingana na Alahmad, mtafiti katika idara ya afya ya mazingira katika Shule ya Chan ya Afya ya Umma ya Chuo Kikuu cha Harvard T.H, kwenye nchi nyingi za kipato cha chini, takwimu za vifo mara nyingi zinaripotiwa kwa wiki au kila mwezi, na sio kila siku.

Anasema hali hiyo inamaanisha kuwa vifo vinavyohusishwa na joto kali havirekodiwi ipasavyo, na hata nchi zenye rasilimali nyingi bado zinapambana kutambua hivyo vitokanavyo na joto.

Mataifa bado hayatunzi takwimu za vifo na athari nyingine zitokanazo na joto kali

Nchini India, kukosekana kwa rekodi sahihi kuhusu vifo vitokanavyo na joto, ni sawa na kushindwa kwa afya ya umma, anasema Dileep Mavalankar, profesa na aliyekuwa mkuu wa taasisi ya Afya ya Umma ya India, kwenye chuo kikuu binafsi katika mji wa Gandhinagar.

Moto wa nyika nchini Macedonia Kaskazini
Mbali ya vigo na magonjwa, wimbi la joto husababisha pia kuzuka kwa moto wa nyika ambao huleta taathira kubwa duniani.Picha: Darko Duridanski/AFP/Getty Images

Kulingana na utafiti wa 2019 uliofanywa na taasisi inayoshughulikia athari zitokanazo na hali ya hewa, inakadiriwa kuwa zaidi ya Wahindi milioni 1.5 watakufa kila mwaka kutokana na joto kali ifikapo mwaka 2100,

Aidha, nchini Mali madaktari katika hospitali ya Gabriel Toure, iliyoko kwenye mji mkuu Bamako, wanasema kuwa takribani wagonjwa 102 walikufa katika kipindi cha siku nne mwezi Aprili, ikilinganishwa na vifo 130 vilivyorekodiwa katika mwezi mzima wa Aprili mwaka 2023.

Vifo hivyo vinahusishwa na kuongezeka kwa joto kali, na matokeo ya kukatika kwa umeme, ambayo yameikumba Mali na nchi nyingine za Afrika katika ukanda wa Sahel ikiwemo Senegal, Guinea, Mali, Burkina Faso, Niger, Nigeria na Chad.

Tunde Ajayi, mtaalamu wa magonjwa na afya ya mazingira, anasema mipangilio ya afya ya Afrika inahitaji kuchanganua takwimu za rekodi ya vifo kutoka katika rekodi za hospitali, ili kuzijulisha takwimu za wizara ya afya na mashirika mengine.

Related Posts