Mwanza. Miili ya watu wawili waliozama maji ndani ya Ziwa Victoria wakati wakitoka Kisiwa cha Yozu kusheherekea ‘Yanga Day’ kuelekea Kitongoji cha Itabagumba, Kata ya Burihaeke wilayani Sengerema imeopolewa.
Miili hiyo ni miongoni mwa watu watano waliokuwa wakitafutwa baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria uliokuwa na watu 23 kuzama maji.
Hata hivyo, watu 17 waliokolewa wakiwa hai, huku mkazi wa Mbugani, Khadija Badru (26) akitolewa majini akiwa amefariki dunia.
Watu hao walizama Agosti 5, 2024 saa 2:00 usiku wakitoka kusheherekea na kuadhimisha Siku ya Wananchi ya Klabu ya Yanga.
Taarifa ya Polisi mkoani Mwanza leo Jumatano Agosti 7, 2024 imesema miili hiyo imeopolewa saa 5:00 asubuhi eneo la Butala kisiwani humo.
Waliopolewa ni Mashauri Ishabakaki (42) mkazi wa Mbugani na Jonathan Mutasyoba (50) mkazi wa Kanyara wilayani Sengerema.
“Jitihada za kutafuta watu wengine watatu zinaendelea ambao ni Masaka Angote (60) Edward Kachelemi (46) na Shija Paschal (30) ambao bado hawajapatikana,”inaeleza taarifa hiyo.
Miili ya marehemu iliyopatikana imekabidhiwa kwa ndugu kuendelea na taratibu za mazishi baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu.