Simulizi ya mama wa mtoto aliyejeruhiwa Goba na dada wa kazi

Dar es Salaam. Siku 24 tangu Malik Hashim (6) alipojeruhiwa shingoni na kitu chenye ncha kali nyumbani kwao Goba, jijini hapa, ameruhusiwa kutoka hospitalini, huku mama yake mzazi akifunguka kuhusu dada wa kazi anayetuhumiwa kumjeruhi.

Timu ya wataalamu 12 ndiyo iliyomtibu Malik katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). Kati ya siku 24 alizolazwa, siku 13 alikuwa chumba cha uangalizi maalumu (ICU).

Akizungumza leo Jumatano Agosti 7, 2024 katika Hospitali ya Muhimbili, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dk Rachel Mhavile amesema Rais Samia Suluhu Hassan amegharimia matibabu ya mtoto huyo.

“Ataondoka kesho (Agosti 8), kisha atakuwa anakuja kila wiki kwa mwezi mmoja kwa ajili ya matazamio kabla ya kuondolewa kifaa maalumu alichofungwa shingoni.

“Tumeshamuelekeza mama yake namna ya kusafisha na kumhudumia mtoto pindi anapokuwa nyumbani,” amesema Dk Mhavile.

Akizungumzia upasuaji wa mtoto huyo, Dk Aslam Nkya, Mkuu wa Idara ya Masikio, Pua na Koo katika hospitali hiyo amesema ulifanyika kwa saa tano, kisha akawekewa kifaa maalumu cha kupumulia.

“Kitu chenye ncha kali kilitenganisha koo na kusababisha njia ya hewa kutengana, lakini kwa kushirikiana na wataalamu wetu wa upasuaji wa shingo, wa usingizi na wauguzi akarudishiwa hali ya kupumua.

“Tunamshukuru Mungu tumefanikiwa kuokoa maisha yake, kwa sasa ataendelea kupumua kwa njia ya koo kwa kutumia Tracheostomy (kifaa maalumu), baadaye tunatarajia atakuwa anatumia mfumo wake wa kawaida wa kupumua,” amesema Dk Nkya.

Daktari mbobezi wa watoto wanaohitaji uangalizi maalumu, Dk Namala Mkopi amesema ushirikiano wa timu zote ndiyo uliomfanya Malik kupona na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Taarifa za Malik kujeruhiwa zilisambaa Julai 16, 2024 kwenye mitandao ya kijamii, huku dada wa kazi nyumbani kwao, Clemencia Mirembe akidaiwa kufanya tukio hilo Julai 15 na kisha kutoroka.

Alikamatwa Julai 21, kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alipokuwa amejificha katika nyumba ambayo haijaisha ‘pagale’.

Shani Charles (30), ambaye ni mama wa Malik amesimulia akisema:

“Ilikuwa saa 12.30 jioni nilipokea simu kutoka kwa jirani yangu mama Zai akiwa Goba. Aliniambia nirudi nyumbani mara moja, Malik amekatwa shingoni.

“Papo hapo nilizima cherehani na kuchukua simu yangu na kuwaambia wenzangu kuwa nakimbilia nyumbani kumuona mwanangu. Namshukuru Mungu, nilipotoka tu ofisini nilikutana na dereva wa pikipiki ambaye alinikimbiza nyumbani,” amesema.

Katika mahojiano na gazeti dada la The Citizen amesema: “Nikiwa naelekea nyumbani jirani yangu alinipigia tena simu na kuniuliza kwa nini nachelewa nitamkuta mwanangu ameshafariki. Nilimwambia niko njiani, nilianza kumuombea mwanangu bila kujua nini kilitokea.”

Amesema alipofika aliona watu wengine wakienda nyumbani kwake, jambo lililomchanganya akatupa simu na viatu akaenda alipokuwa mwanaye.

“Nilimkuta mwanangu wa pekee amefunikwa na mtandio. Nilimshika na kwenda moja kwa moja kwenye pikipiki niliyokuja nayo na kumtaka anikimbize B2B, hospitali binafsi ya Goba,” amesimulia.

Amesema njiani alikuwa akimweleza mwanaye asilale huku akimuombea. “Nilimuuliza ni nani aliyekufanyia hivi, akasema kwa sauti ya chini sana na kwa uchungu dada, akimaanisha mfanyakazi wetu wa zamani wa nyumbani Clemensia Mirembe (19),” amesema.

Amesema baadaye alishindwa kuendelea kuzungumza na kwa kutumia tochi ya simu aliangalia jeraha wakiwa njiani.

“Niligundua alikatwa nyuma ya shingo na koo lake, alipopumua hewa ilikuwa ikitoka tu. Nilipiga kelele na kumwambia dereva atupeleke haraka hospitali. Tulipofika nilikuwa napiga kelele tu na kuomba msaada. Ndipo nilipogundua mwanangu hakuwa na nguo,” amesema Shani.

Amesema walipewa rufaa kwenda Muhimbili siku hiyohiyo, saa 3 usiku.

Amemshukuru Rais Samia kwa kugharimia matibabu ya mwanaye pamoja na wafanyakazi wa Muhimbili kwa kujitolea kwao.

Akizungumzia uhusiano wao na mfanyakazi wa ndani, amesema Malik na dada huyo walikuwa na uhusiano mzuri na mpaka sasa mwanaye anamuulizia.

Familia hiyo imeishi na Clemencia kwa takriban miezi saba, jambo linalowashangaza Shani na mumewe, Hashim Kitumbi nini kilimpata dada huyo kwa kuwa hakukuwa na tatizo baina yao hadi siku ya tukio.

“Kwa kweli sijui nini kilimpata Clemensia. Yeye ni mtu mzuri na tulikuwa na uhusiano mzuri. Sitaki tu kuamini kwamba alifanya hivyo kwa akili yake timamu. Muda mwingi alikuwa akimkumbatia mwanangu wakiwa wamelala, hakuwahi kumwachia acheze mbali na macho yake,” amesema.

Akijibu swali iwapo alimfahamu vyema Clemencia kabla ya kumuajiri, amesema hakumfahamu bali alitambulishwa na mtu anayemfahamu.

Shani amesema mara kwa mara alikuwa akiiangalia simu ya Clemencia na kuona mazungumzo yake na ndugu zake ambayo yalikuwa ya kuomba msamaha bila kueleza alichowafanyia.

Amesema alipomuuliza, alimweleza kuwa hakuelewana na dada yake wa Morogoro na kuna wakati aliomba nauli ya basi aende Morogoro kumuomba msamaha, jambo ambalo hakuwahi kulifanya hata baada ya kupewa nauli.

“Sitamwajiri tena mfanyakazi wa nyumbani katika maisha yangu, kwani sitamuamini mtu yeyote,” amesema.

Amesema maisha yao baada ya matibabu ni changamoto, akieleza mwanasaikolojia aliwaambia wanatakiwa kuondoka nyumbani kwao kwa takribani miezi minne, ili mtoto asahau yaliyompata.

“Changamoto ni kwamba hatuna mahali pa kwenda. Bado tunatafuta tuelekee wapi, kwani nyumba ya Goba ni yetu. Kupata mahali pa kuishi ni changamoto. Yeyote anayeweza kutusaidia mahali pa kuishi tutamshukuru,” amesema.

Baba mzazi wa Malik amesema, “kwa sasa tuna kipindi kigumu, tunaomba msaada tubadilishe mazingira ya nyumbani ili iondoe kumbukumbu kwa mtoto anaporudi hivi sasa asikumbuke alishafanyiwa ukatili mahali hapo.”

Imeandikwa na Sute Kamwelwe, Victoria Michael na Salome Gregory

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts