WANAKC,WANAGDSS WATAKIWA KUPAZA SAUTI KUELIMISHA JAMII KUSHIRIKI UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

VITUO vya Taarifa na Maarifa (KC) na wanaGDSS wametakiwa kupaza sauti zao kuhakikisha jamii inapata uelewa mkubwa na kuweza kujitokeza kujiandikisha kwneye daftari la kudumu la wapiga kura ili kuweza kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Vilevile wametakiwa kutengeneza ajenda ambayo itasukuma jamii kujitokeza kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa ili waweze kupiga kura na kuchagua viongozi bora ambao watawaongoza katika maeneo yao.

Wito huo umetolewa leo Agosti 7, 2024 wakati wa Semina za Jinsia na Maendeleo ambazo hufanyika kila Jumatano ya wiki katika viwanja vya TGNP- Mtandao Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika Semina hizo Mwasilishaji wa Mada, Shufaa Seilogo amesema kuna umuhimu mkubwa jamii ikatambua umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa ili kuhakikisha tunapata viongozi wenye uwazi na uwajibikaji.

Amesema kiongozi ambaye atachaguliwa anatakiwa kutambua haki za kijinsia, usawa wa kijinsia pamoja na kutambua masuala mazima ya kijamii ikiwemo changamoto za miundombinu pamoja na kusikiliza kero kutoka kwa wananchi.

Aidha amesema kuna umuhimu wa kuchagua viongozi bora wa serikali za mitaa kwani watasaidia kuleta maendeleo kwenye jamii kwa kusogeza huduma muhimu na ambaye atakuwa mwakilishi na mbeba maoni ya jamii na kutoa tamko.

Kwa upande wake Mdau wa Semina za Jinsia na Maendeleo Wenslaus Kidakule amesema kupitia mafunzo ambayo wameyapata watakwenda kuelimisha jamii kuhusu umuhimu mkubwa wa kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kuweza kupata viongozi ambao watawaongoza.

Amesema wao kama wanaharakati, kupitia shughuli ambazo wanazifanya katika kuleta maendeleo watatengeneza ajenda mahususi ambayo itaweza kusaidia kuifikia jamii kwa urahisi katika kutoa elimu juu ya umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa.














Related Posts