Sauti alivyogeuza changamoto soko la nyanya kuwa fursa

Dodoma. Upo msemo kuwa “Ukiona vinaelea vimeundwa”, ukiwa na maana ukiona jambo zuri basi kuna watu wameliwezesha kufikia hapo.

Maisha ya Imani Sauti (27), mkazi wa Kata ya Ludewa iliyopo Kilosa mkoani Morogoro yanaendana na msemo huo wa wahenga, hasa ukiangalia maisha yake ya sasa na njia alizozitumia kufikia hapo.

Baada ya kuhitimu kidato cha nne, Sauti  hakufanikiwa kuendelea na masomo kutokana na ufaulu wa chini, lakini hilo haikumkatisha tamaa, aliungana na wazazi wake katika shughuli za kilimo cha nafaka na mbogamboga.

“Kwa sehemu kubwa nilikuwa nikiwasaidia wazazi wangu katika kilimo, maana nilikuwa nalima robo eka na baada ya kuvuna napata Sh100, 000, jambo ambalo halikunipa mwelekeo wa maisha,” anasema Sauti.

Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi Digitali leo Aprili 27, 2024, Sauti amesema akiwa anaendelea na shughuli za kilimo, alisikia habari za Mradi wa Fursa za Ajira (OYE) kupitia ofisi za kijiji naye akaenda.

Katika mradi huo, anasema alipata mafunzo ya kujitambua, namna ya kuwasiliana na watu, kutambua changamoto na namna ya kuzitatua pamoja na namna ya kujiwekea akiba katika shughuli anazozifanya.

“Pia tulijifunza tunavyoweza kujikwamua kimaisha, kuwa na nia katika unachotaka kufanya, kubadili changamoto kuwa fursa na kwenye stadi za kazi tulifundishwa kilimo cha mbogamboga, matunda na nafaka,” anasema.

Anasema baada ya mafunzo hayo, alianza moja kwa moja kilimo cha mbogamboga, akilima bamia na nyanya pamoja na nafaka, mahindi na maharage.

Anasema kwa kuwa alishapata ujuzi, aliwaomba wazazi wake mtaji wa Sh200, 000 kwa ajili ya kununua dawa na mbolea kwa ajili ya kilimo hicho.

“Nilikuwa nafanya kazi zote mwenyewe kwenye shamba langu, nikiwa kama kibarua na mmiliki. Hapa nilikuwa naangalia kupata mtaji zaidi ili niweze kuwa na shamba kubwa  na kupanua kilimo change, ndipo nikafanikiwa kupata mtaji wa Sh900,000,” anasema.

Anasema bidii aliyoiweka katika shamba hilo, ilimwezesha kuongeza mtaji kutoka Sh900,000 hadi kufikia Sh2 milioni, fedha ambazo alizitumia kuongeza mashamba kwa kununua na kukodisha.

Anasema baadaye alifanikiwa kununua shamba la ekari tatu alilolitumia kulima mahindi na maharage huku akiongeza ukubwa wa shamba la mboga mboga kutoka robo eka hadi robo tatu ya eka.

“Pia nilijiunga na vikundi vya kuweka na kukopa ambavyo vilinisaidia sana nikikwama kusafirisha mazao nakopa na kupeleka mazao yangu,” anasema.

Anasema mafunzo aliyoyapata kutoka kwenye mradi OYE, yamemsaidia kujisimamia badala ya kuwa tegemezi na sasa ana mwanga wa kukua kiuchumi.

Sauti anasema changamoto za kukosa soko zilimfanya kufikiri zaidi jinsi anavyoweza kukabiliana nazo ili kuondokana na hasara.

Anasema changamoto hiyo huanza kati ya Juni na Julai kila mwaka, baada ya wakulima kuvuna mazao ya nafaka na kugeukia kilimo cha mbogamboga.

“Debe moja la nyanya katika kipindi ambacho zinakuwa nyingi sokoni, huwa ni Sh5,000, ukiuza hivyo unapata hasara. Lakini wakati mwingine ambapo hakuna nyanya nyingi, tunaliuza Sh28,000,” anasema Sauti.

Anasema hali hiyo ilimfanya aombe kwenye mradi wa OYE mafunzo maalumu ya usindikaji wa nyanya kwa kutengeneza ‘tomato source’, jambo ambalo alifanikiwa na kupata mafunzo ya wiki mbili.

Anasema alipotoka kwenye mafunzo hayo, alianza kutengeneza mchuzi wa nyanya pale zinapokuwa nyingi sokoni, kiasi ambacho kinasababisha hasara kwa mkulima.

Anasema kwa sasa chini ya Mtandao wa Usimamizi wa Misitu Tanzania ambao ni miongoni mwa watekelezaji wa mradi wa OYE, anauza nyanya katika soko la kijijini kwake kwa Sh2,000 kila lita ya tomato source.

Anasema bidhaa hiyo inadumu kati ya mwaka mmoja hadi miwili bila kuharibika na sasa anafikiria kusajili jina na kiwanda chake kidogo.

Mafanikio mengine anayojivunia ni kununua pikipiki ambayo anaitumia kuzungukia mashamba yake aliyokodisha yanayofikia eka tano na kubebea bidhaa kwa ajili ya kupeleka sokoni.

Sauti ambaye alianza kilimo hicho akiwa na umri wa miaka 26, anawashauri vijana wenzie wawe na malengo na nia ya kutumia fursa yoyote wanayokutana nayo, badala ya kusubiri kile wanachopenda kukifanya.

“Kuna shughuli wanaweza kufanya na wakapata fedha na kujikwamua kidogo kodogo kiuchumi huku wakisubiri kifike kile wanachopenda kukifanya. Tuondoe dhana kuwa hiki sikiwezi bali shughuli fulani ndio naiweza,” anasema.

Sauti anaweza kuwa ni mwakilishi wa maelfu ya vijana waliombolewa na mradi wa OYE, ikiwa na wao walijituma na kujiongeza.

 Meneja Mradi wa Fursa za Ajira (OYE) wa Shirika la SNV, Tanzania, Bonavitha Gahaini anasema awamu ya pili ya mradi huo iliyoanza Aprili 2021 na Machi mwaka 2024, ilikuwa na lengo la kuboresha maisha ya vijana 4,250, wenye umri kati ya miaka 18 hadi 30 waliopo vijijini na pembezoni mwa miji.

“Mradi huu ulikuwa katika mikoa miwili ya Morogoro na Singida. Awamu ya pili ya OYE iliendelea kuweka kipaumbele kwa vijana walio nje ya shule kama kundi kuu lengwa,” anasema.

Akifunga mradi huo, Mkurugenzi Msaidizi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Eliakim Mtawa, amewataka vijana walionufaika na mradi huo kuendeleza miradi, makongamano na vikundi vya kuweka na kukopa, walivyovianzisha kwa kuwa vitakuwa vyenzo za kupata mitaji kwenye taasisi za kifedha.

Related Posts