MTU WA MPIRA: Kwa Simba hii hata apewe Gamondi haifanyi maajabu

Nimeona mitandaoni tetesi Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha ameomba kuondoka mwishoni mwa msimu. Sijui kama ni ukweli ama uongo maana waandishi wengi wa kizazi cha sasa wanapenda zaidi ‘umbea’.

Hata hivyo, mambo mengi yanayosemwa kwenye soka letu huwa ni kweli. Japo hili la Benchikha tunapaswa kujiridhisha zaidi.

Japo jambo la uhakika ni kwamba Benchikha lazima angetoa mapendekezo makubwa mwishoni mwa msimu. Kama siyo kuondoka lazima angeomba marekebisho makubwa ya kikosi chake.

Kikosi cha Simba cha sasa kina uwezo mdogo sana. Kinaundwa na makundi matatu ya wachezaji wenye changamoto tofauti. Halafu wanabaki wachache wenye nafuu.

Kundi la kwanza ni la wachezaji mahiri ambao umri umekwenda. Hawa ndio kina Clatous Chama, Saido Ntibazonkiza, Shomari Kapombe, John Bocco, Mzamiru Yassin na wengineo.

Ni wachezaji ambao wamewahi kufanya makubwa na Simba ama kwingineko walikopita. Walicheza kwenye kiwango bora sana katika wakati wao.

Hata hivyo, kwa sasa akili inataka Ila mwili umechoka. Hawawezi kukimbia tena sana kama zamani. Hawana msaada mkubwa timu inapokuwa haina mpira. Ndio sababu kila Simba inapopokonywa mpira mambo yanakuwa magumu.

Kundi la pili ni wachezaji wenye umri sahihi ambao hawana uwezo mkubwa. Ndio hawa kina David Kameta ’Duchu’, Israël Mwenda, Edwin Balua, Leandre Onana, Pa Omary Jobe na wengineo. Hawa wako katika umri sahihi lakini uwezo walionao ni wa kawaida.

Wakipewa nafasi wanacheza kitoto. Wanapoteza mipira ovyo. Hawakai kwenye mpango wa mwalimu. Yaani wanaonekana hawana la maana sana wanalofanya kuliko hata wale wazee.

Kundi la tatu ni la wachezaji ambao walikua mahiri wakati fulani, lakini sasa wameshuka viwango. Walicheza kwenye ubora wa juu wakiwa Simba ama timu nyingine lakini sasa hawana jipya sana.

Ndio hawa kina Luis Miquissone, Fabrice Ngoma, Babacar Sarr na wengineo. Hawa wanabebwa tu na kile walichofanya zamani lakini kwa sasa uwezo wao uwanjani ni wa kawaida. Hawana mpya sana.

Halafu baada ya hapo wapo wachache wenye uwezo ambao unaendana na mahitaji ya Simba sasa. Kina Che Malone, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’, Sadio Kanoute, Henock Inonga, Ayoub Lakred na wengineo.

Hivyo unaposikia Benchikha ameomba kuondoka kwa madai Simba haiwezi kumjenga vizuri na kushindana Afrika unaelewa. Yawezekana sio ukweli ameomba kuondoka ila ukweli ni kwa Simba hii hata angeshuka Nabii Musa wala isingekuwa na maajabu.

Simba hii ndio inafanya tumuone Benchikha kama kocha wa kawaida. Atafanya nini zaidi ya anachofanya sasa? Hakuna.

Nilimtazama kwenye mechi ya Dabi ya Kariakoo. Maelekezo mengi aliyokuwa anatoa wachezaji hawakuwa wanayafanyia kazi. Kila mtu alicheza zaidi kivyake.

Makosa mengi waliyofanya Simba ilikua tofauti kabisa na maelekezo aliyokuwa akiwapa kocha wao. Wachezaji walitamani kufanya zaidi, lakini uwezo wao uliishia pale.

Ndio maana nasema licha ya kwamba tunamwona Miguel Gamondi kuwa kocha bora kwenye Ligi yetu kwa sasa bado akipewa hii Simba tutamkataa.

Yanga ya Gamondi inaundwa na wachezaji wengi wenye uwezo karibu kila sehemu. Wapo kwenye umri sahihi, wana kasi na ubunifu.

Mfano viungo wa Yanga, Mudathir Yahya, Khalid Aucho, Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua na wengineo utawafananisha na wachezaji gani pale Simba? Hakuna.

Huyo Maxi Nzengeli ni kama turufu ya mfumo wa Gamondi. Kila anachoelekezwa anafanya kwa ufasaha.

Mechi dhidi ya Mamelodi Sundowns kuna muda alikuwa beki na wakati mwingine akawa mshambuliaji.

Eneo ambalo lina changamoto kote ni mshambuliaji wa mwisho. Joseph Guede ni kama Freddy Michael wa Simba tu. Hawana mpya sana.

Lakini kwa Yanga huwezi kuona tatizo kubwa maana viungo wanafunga.

Simba nani anafunga? Kibu Denis, Miquissone? Saido? Hakuna. Viungo wa Simba wamechoka ila wa Yanga wamechangamka.

Ndio sababu nasema hata leo Gamondi akienda Simba tutamuona kituko. Benchikha akienda Yanga anaweza kuwa kocha bora wa msimu na kufika mbali zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hivyo wakati huu tunasikia tetesi za Benchikha kuondoka wala tusishtuke sana.

Ila hata akibaki basi kikosi cha Simba kitafanyiwa mabadiliko makubwa sana.

Related Posts