NIONAVYO: Riadha yetu inahitaji kazi ya ziada

WIKIENDI iliyopita Jumamosi na Jumapili, Jiji la Dar es Salaam na nchi kwa jumla kulikuwa na shamrashamra na mashamushamu kutokana na matamasha mawili makubwa ya klabu maarufu za Simba na Yanga.

Matamasha hayo yalijaza uwanja likiwamo la Yanga ambalo mashabiki walilazimika kutumia Uwanja wa Uhuru baada ya ule wa Benjamin Mkapa kujaa.

Kulikuwa na matukio mengi kwenye matamasha hayo ikiwamo muziki, utambulisho wa wachezaji na jezi za msimu mpya 2024/25 pamoja na michezo ya kirafiki kwa miamba hiyo ya soka na ni wazi walioshuhudia walipata picha kwamba Tanzania ni nchi ya wanamichezo.

Hata hivyo, wakati hayo yakifanyika ikiwamo michuano ya Ngao ya Jamii iliyopigwa kuanzia jana, jijini Paris, Ufaransa michezo ya Olimpiki inaendelea na baadhi ya washiriki kutoka Tanzania wameenda kuliwakilisha taifa, lakini hakuna dalili ya kuibuka kidedea.

Ni kweli kesho Jumamosi wanariadha wetu wawili wa kike, Magdalena Shauri na Jackline Sakilu watakimbia mbio ndefu za marathoni baada ya wanamichezo wenzao watatu, Collins Saliboko na Sophia Latiff wa kuogelea na Andrew Thomas Mlugu wa Judo kutolewa mapema katika michezo hiyo.

Pia, Jumapili wakati wa ufungwaji wa michezo hiyo, nahodha wa timu ya Tanzania, Alphonce Simbu na mwenzake, Gabriel Geay watakimbia pia Marathon kwa wanaume na kila Mtanzania atakuwa anawafuatilia kuona wanaibeba vipi nchi kabla ya timu kurejea nyumbani.

Watanzania walio wengi wamekata tamaa mapema kwa wanamichezo wawakilishi wa nchi kutokana na aina ya maandalizi kulinganisha na mataifa mengine.

Pia hata idadi ya washiriki katika Olimpiki ya Paris kwa taifa letu ni ndogo kulinganisha na mataifa mengine ambao yametuma wanamichezo zaidi ya 100 ambao wameanza kuona matunda kwa kuzoa medali za kumwaga.

Mataifa kama China, USA, Australia na wengine wanazoa medali, sisi macho kodo. Ni miaka mingi imepita tangu wawakilishi wetu katika michezo hiyo mwaka 1980, Filbert Bayi na Suleiman Nyambui kubeba medali za fedha zikiwa ni za pekee kwa taifa hili.

Ni muda wa kufikiria namna ya kuongeza nguvu katika kuandaa na kukuza vipaji vya kuja kutuletea medali tena katimja michezo hiyo na mingine ya kimataifa. Hakuna njia ya mkato ya kufikia mafanikio. Kama wanamichezo wengine, wanariadha wanaandaliwa.

Maandalizi ya mwanariadha hayafanyiki katika saa 24 bali ni kazi ya miaka mingi tangu umri mdogo na watoto wanatakiwa waandaliwe tangu umri wa kwenda shule na waendelee kufundishwa na kushindanishwa huku malengo yakiwa kuwafikisha kiwango cha dunia.

Zimeondoka siku za magwiji Filbert Bayi, Gidamis Shahanga, Suleiman Nyambui na wengineoi wa wakati ule. Si shuleni wala majeshi ama mtaani tunakozalisha wanariadha nguli. Si kwamba Watanzania hawana vipaji, hapana. Tunawekeza zaidi katika kuonyesha matokeo kuliko kutengeneza matokeo.

Hata soka tunalojivuna nao, bado unategemea zaidi uwekezaji wa juu kuliko uwekezaji wa mashinani. Klabu zetu zinategemea kutumia fedha nyingi kununua vipaji vilivyoandaliwa nje kuliko vipaji vilivyotengenezwa nchini.

Medali wanazozoa Waafrika wenzetu wa Kenya, Afrika ya Kusini, Ethiopia, Algeria na wengine haziji kama kuokota embe chini ya mti wa mwarobaini, hapana! Zimetafutwa kwa mikakati ya muda mrefu.

Kama tunataka mafanikio katika riadha, tunatakiwa kuandaa mazingira tangu shuleni, kuandaa wataalamu, miundombinu bora na zaidi kutenga fedha za uwekezaji katika sekta hiyo muhimu.

Mchezo wa riadha unalipa, mchezo wa riadha unatangaza nchi. Kupitia matokeo ya Olimpiki ya Paris tunatakiwa kujisahihisha, kufungua macho na kutengeneza mkakati thabiti wa maendeleo ya riadha. Lakini kubwa kuongeze dua zetu kwa wanariadha wanne walioshikilia hatma ya Tanzania kwa sasa. Inawezekana.

Mwandishi wa makala haya ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kwenye simu yake hapo juu.

Related Posts