Dar es Salaam. China imetoa fursa ya Watanzania nchini kupata ufadhili wa kusomeshwa katika Taifa hilo la pili kiuchumi na kwa idadi ya watu duniani.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam inayofundisha lugha ya Kichina (CI), Profesa, Zhang Xiaozhen, wakati wa kukabidhi msaada wa vitabu 100 kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mtakatifu Mathew iliyopo Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani.
Taasisi imetoa vitabu hivyo kwa kushirikiana na Kampuni ya Ujenzi inayomilikiwa na Serikali ya China (CCCC) ili kujifunza lugha ya Kichina
Amesema kuna awamu sita za kujifunza lugha ya Kichina na mtu anayefikia awamu ya tatu anaweza kuomba ufadhili wa kwenda kusomea nchini China
“Taasisi hii imekuwa ikifundisha lugha ya Kichina, mpaka sasa wanafunzi 100 wamenufaika kwa kujifunza na wengine wamepata ufadhili wa masomo ya elimu ya juu nchini China,” amesema Xiaozhen.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtakatifu Mathew, Joseph Nalaila, amesema kutokana na kukuwa kwa utandawazi duniani ili mtoto aweze kufanikiwa ni vema akajifunza lugha mbalimbali ikiwemo ya Kichina.
Amesema China ni kati ya nchi zinazokua kwa kasi kiuchumi, kibiashara na lugha ya Kichina inatumika sana, “hivyo tumeona watoto wetu ili waweze kufanikiwa zaidi katika maisha yao, wanasoma masomo ya darasani kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha sita pamoja na hayo wanasoma lugha ya Kichina.
“Watoto 100 wamenufaika kwa kujifunza lugha ya Kichina na wengine wamepata ufadhili wa kusoma China, wafanyabiashara wakubwa wanakwenda China na kurudi tumeona lugha ya Kichina ina mafanikio,” amesema Mwalimu Nalaila.
Naye Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Peter Mutembei amesema wameweka nguvu kubwa kuhakikisha wanafunzi kuanzia shule ya msingi hadi sekondari wanafundishwa lugha ya Kichina kwa ufasaha, ili kuwawezesha kuwa washindani katika dunia ya sasa.
“Tunahakikisha tunatafuta fursa zozote ambazo zipo zitakazowawezesha watoto wetu kufanikiwa katika ulimwengu wa sasa na fursa mojawapo ni kufahamu lugha ya Kichina. Huwezi kukwepa lugha ya Kichina kutokana na namna walivyowekeza katika dunia ya sasa,” amesema Mutembei.
Mmoja wa wanafunzi wa kidato cha kwanza shuleni hapo anayesoma lugha ya Kichina, Rahel Samweli amesema amevutiwa kujifunza ili aweze kuwa na uwanda mpana wa kuelewa lugha za mataifa mbalimbali.