Mbeya. Baada ya siku kadhaa tangu Mwananchi kuripoti kuhusiana na taarifa za kutoweka kijana, Shadrack Chaula (24) aliyetuhumiwa kuchoma picha ya Rais Samia Suluhu Hassan, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamini Kuzaga amevunja ukimya.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana Agosti 8,2024, Kamanda Kugaza amekiri kuwepo kwa tukio la kutoweka kwa kijana Shadrack huku akiomba wananchi kutoa ushiriano.
‘Taarifa ya Kuzaga imeeleza kuwa baba mzazi wa Shadrack, Yusufu Chaula (56) alitoa taarifa ya kutoweka kijana wake Agosti 2, mwaka huu akiwa katika shughuli zake katika Kijiji cha Ntokela Kata ya Ndato Wilaya ya Rungwe.
“Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kwa sasa wako katika uchunguzi kujua watu waliomchukua na kuomba wananchi kutoa ushirikiano ili aweze kupatikana” imesema taarifa hiyo.
Shadrack hapo awali alihukumiwa kulipa faini ya Sh5 milioni au kifungo cha miaka miwili jela baada ya kukiri kosa la kuchoma picha ya Rais.
Kijana huyo alikwepa kifungo hicho baada ya wananchi kuchanga na kulipa faini hiyo ya Sh5 milioni na kufanikiwa kumtoa katika Gereza la Ruanda Mkoa lililoko mkoani Mbeya.
Endelea kufuatilia Mwananchi.