AKILI ZA KIJIWENI: Wanawake wameamua kupambania fursa za soka

NI jambo la kupendeza kuona idadi kubwa ya wachezaji wa soka la wanawake inaenda kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania katika siku za hivi karibuni.

Tumeona juzi timu ya wanawake ya Brighton inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake ya England ilimsajili Aisha Masaka ambaye kabla ya hapo alikuwa Sweden akiichezea BK Hacken.

Muda mfupi baada ya Masaka kutua Brighton, nahodha katika timu ya taifa ya soka ha wanawake Tanzania ‘Twiga Stars’, Opah Clement alijiunga na Henan Jianye ya China akitokea Besiktas ya Uturuki.

Uhamisho uliofuata baada ya hapo ni ule wa beki Noela Luhala aliyekuwa akiichezea Yanga Princess aliyejiunga na ASA Tel Aviv ya Israel kama mchezaji huru baada ya mkataba wake na Yanga kumalizika.

Ukiondoa hao kuna wengine ambao wapo nje ya nchi wakisakata kabumbu la kulipwa kama vile Julitha Singano, Diana Msewa, Enekia Kasonga na Clara Luvanga na wote wana uhakika wa namba kwenye timu zao.

Ndiyo maana leo sio jambo la kushangaza kuona Twiga Stars ikiwa na kikosi cha kwanza chenye wachezaji wasiopungua watano wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi tofauti na zamani hawakuwepo.

Huu ni uelekeo mzuri na wenye maana kubwa kwa soka la wanawake hapa nchini ambalo limekuwa likipiga hatua kubwa siku hadi siku na ushindani wake kukaribia kufanana na ule wa wanaume.

Wanawake wanasoka badala ya kusubiri kuwezeshwa, wamejivika vazi la ujasiri, utayari na uthubutu na kusaka fursa nje ya Tanzania ambako wanapiga noti za kutosha na wanapata mazingira bora ya kukuza vipaji na majina yao.

Related Posts