Kikosi cha Yanga jioni ya jana kilikuwa uwanjani kumalizana na Coastal Union katika mechi ya Ligi Kuu Bara, huku mastaa wa timu hiyo, Djigui Diarra, Maxi Nzengeli na Stephane Aziz KI walitarajiwa kuendeleza moto ulioifanya timu hiyo iwe tishio kwa sasa mbele ya wapinzani wanaochuana nao kuwania ubingwa.
Hata hivyo, sasa unaambiwa tofauti na unavyowaona mastaa hao na wengine wa timu hiyo akiwamo Pacome Zouzoua ambaye hajaonekana uwanjani tangu pambano la Yanga na Azam FC, wana maisha fulani ya aina yake kambini na inaelezwa maisha hayo yamechangia kuifanya timu hiyo iwe hivyo ilivyo yaani fulu ushirikiano.
Kabla ya mechi hiyo ya jana, Yanga ilikuwa kileleni na pointi 59 baada ya mechi 23 ikiziacha Azam ya pili na alama zao 55 baada ya mechi 24 na Simba ikishika nafasi ya tatu na pointi 46 kwa michezo 21 na usiku wa jana timu hizo mbili zinazowafuata watetezi hao wa Ligi Kuu, zilikuwa uwanjani katika fainali ya Kombe la Muungano lililohitimishwa jana mjini Unguja.
Yanga ilichomoa kushiriki michuano hiyo iliyoshirikisha timu nne zikiwamo KVZ na KMKM zilizotolewa mapema kwenye nusu fainali mbele ya Simba na Azam.
Sasa unaambiwa, mastaa walio ndani ya kikosi hicho wametoka mataifa tofauti kuna Tanzania, DR Congo, Mali, Ivory Coast, Burkina Faso, Ghana, Uganda, Zambia na Afrika Kusini.
Mchanganyiko wa mataifa hayo kila mchezaji ana tabia zake na Mwanaspoti limefanya mazungumzo na Meneja wa Yanga, Walter Harrison aliyefunguka tabia za baadhi ya wachezaji wa timu hiyo na jinsi ambavyo kambi ya timu hiyo iliyopo Avic Town, Kigamboni inavyonoga na kuwafanya wote kujiona kama familia moja.
Achana na namna anavyowaongoza wachezaji wenzake uwanjani akiwa langoni, unaambiwa namna anavyofanya kazi kwa ukaribu na wenzake hadi nje ya uwanja ni hivyo hivyo.
“Diarra ni mwema sana, naomba kumfananisha kama mzazi nyumbani kwa sababu ni mtoaji, habagui, hapendi kuona mtu analia shida akiwa na uwezo na hiyo shida anaifanyia kazi,” anasema Walter na kuongeza;
“Ukiachana na hilo, pia ni mtu ambaye akisafiri kwenda nje lazima akumbuke zawadi za wenzake mfano makipa wenzake wanafaidi kwenye zawadi za glove na hata wachezaji wengine pia wataletewa manukato.”
Unadhifu wake unaanzia uwanjani ukimwona lazima utabaini utofauti na wenzake hawezi kucheza bila kuchomekea basi unaambiwa staa huyo nje ya uwanja pia anapenda kuonekana tofauti kwa kupendeza.
“Ni nadhifu sana na anapenda kutupia. Ndani kwake kuna rundo la nguo, kwani huwezi kumkuta anarudia nguo moja zaidi ya mara moja, anapenda kuwa na muonekano mzuri pia ni mtu ambaye anapenda kujifunza,” anasema Walter.
JOYCE LOMALISA- YEYE NA SIMU
Wanamwita Waziri wa Maji kutokana na namna ambavyo amekuwa akitoa pasi zake kutokea pembeni. Basi unaambiwa nje ya uwanja ni mtu wa simu muda mwingi.
“Hana mambo mengi na sio mtu wa stori na wenzake, mazungumzo na wachezaji wenzie ni uwanjani tu baada ya hapo yeye muda mwingi ni simu tu,” anasema.
Nahodha wa Yanga kwa misimu minne tangu ametua Yanga akitokea Coastal Union, Bakar Mwamnyeto unaambiwa ni fundi wa kuahirisha mambo, sio mnyoofu kuanzia kwenye muda hadi utekelezaji.
“Mnaweza mkapanga jambo, lakini baadae akatafuta sababu ili liweze kubadilishwa hilo jambo. Napenda kumuita miyeyusho flani,” anasema Walter huku akicheka, licha ya kukiri kwenye utekelezaji wa majukumu yake mengine yupo siriazi kama anavyoonekana uwanjani.
Kitasa wa Yanga hivyo ndio wanamuita sasa baada ya kujihakikishia namba kikosi cha kwanza kutokana na ubora wake. Unaambiwa staa huyo uwanjani yupo makini sana na anafanya kazi kwa usahihi.
“Sio mtu wa mchezo awapo uwanjani. Nje ya uwanja ni miyeyusho sana, ni mtu wa maneno mengi utekelezaji mdogo sana kama ilivyo kwa Mwamnyeto.”
DICKSON JOB-RAFIKI WA WOTE
Ni nahodha msaidizi wa Yanga, imefichuka pia sababu za kupewa nafasi hiyo ni kutokana na namna ambavyo amekuwa karibu na kila mtu ni mtu ambaye habagui nani wa kuzungumza naye.
“Ni mtu wa watu na amekuwa rafiki wa kila mtu kuanzia benchi la ufundi hadi wachezaji. Ukiachana na ukaribu wake na Kibwana Shomari, Aboutwalib Mshery na Nickson Kibabage kutokana na makuzi yao tangu wakiwa Morogoro na walipoibuka katika soka, yeye ni mtu wa watu,” anasema Walter.
Ufundi wake uwanjani akipiga pasi za kuaminika ambazo zinafika kwa mlengwa ni hivyo hivyo kwenye maisha yake ya kawaida. Aucho anaelezwa ni mchezaji ambaye hana maneno maneno na muda mwingi anapenda kuwa mwenyewe.
“Aucho ni mchezaji ambaye muda mwingi anajifungia ndani huwezi kuingia chumba chake bila ya ruhusa yake kwani ni mtu ambaye amekuwa akijifungia sana ndani peke yake,” anasema.
Anapenda kucheka hata ukikutana naye, mara zote yeye na tabasamu basi na unaambiwa hadi kwenye jambo ambalo ni la maana anafanya utani kwa kucheka.
“Sure Boy muda wote anafanya matani hadi kwenye mambo ya msingi. Kicheko kwake kwanza halafu mambo mengine yanafuata. Kifupi ni mcheshi sana,” anasema meneja wa Yanga.
Sio mchezaji ambaye anapata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza, lakini hilo wala hajali kwani anaangalia moyo wake unapata furaha kwa jambo gani, basi kwake Nkane picha tu.
“Anapenda picha kila eneo alilopo yeye ni kujiweka tayari kwa ajili ya picha, pia ni mcheshi sana na amekuwa kipenzi cha wachezaji wengi hasa wa kigeni kwa sababu anapata nafasi ya kuwafundisha vitu mbalimbali,” anasema.
Ukimwona kwa ukaribu unaona mchezaji mpole na mwenye aibu, lakini ukweli, anapokuwa kambini kumbe wala sivyo alivyo na Walter anasema ukitaka kufurahi ndani ya kikosi cha Yanga sasa basi kaa karibu na Farid.
“Ni mchezaji ambaye ni mcheshi na mchekeshaji pia anapenda sana kuwatisha wachezaji wenzake kambini kwa sababu anapenda kuangalia filamu za kutisha, hivyo kwa wachezaji waoga basi wanamkimbia,” anasema.
Achana na kuonekana kwake kila eneo awapo uwanjani akiipambania timu yake, unaambiwa winga huyo yupo smati kuanzia mazoezini hadi muda wa kula.
“Maxi anapenda mazoezi. Ndiye mchezaji wa kwanza kufika uwanja wa mazoezi na ni mchezaji wa kwanza kufika eneo la kula, hivyo ana nidhamu mazoezini na sehemu ya kula ni kama mlokole fulani hivi asiyependa tabu na mtu,” anasema.
Achana na kipaji kikubwa cha soka alichonacho, Pacome Zouzoua wa kambini ni mtu mwingine kabisa na asiyechangamana sana na wenzake.
Inaelezwa lugha ndio changamoto kubwa kwake na hawezi kuzungumza Kiingereza wala Kiswahili amekuwa akizungumza Kifaransa, hivyo muda mwingi anakuwa karibu na watu wanaomwelewa zaidi.
“Na ndio maana muda mwingi anaonekana na Yao pamoja na Aziz Ki. Shida ni lugha tu, lakini ni mcheshi na anapenda ushirikiano,” amesema Walter meneja wa Yanga ambaye muda mwingi anakaa na wachezaji.
Kinara wa upachikaji wa mabao Ligi Kuu na Yanga, yeye majukumu bora ni uwanjani atakupa kila kitu atafunga na kutoa pasi za mwisho lakini nje ya hapo ni ucheshi na utoaji.
“Hajui kuimba wala kucheza muziki, kazi yake bora ni uwanjani lakini ni mchezaji ambaye ni mtoaji sana na ana upendo sana,” anasema.
MUDATHIR YAHYA- NI MKEWE TU
Kwa sasa anazungumzwa zaidi kutokana na kutupia kwake na kuwa na staili yake ya ushangiliaji ya kupiga simu na kuweka wazi kuwa ni maalum kwa mkewe.
“Mudathir anampenda sana mkewe na muda mwingi anautumia kuongea naye pia ni Mcha Mungu kwa upande wa wachezaji wa Kiislam, yeye ndiye amekuwa akiswali sana sambamba na Aucho,” anasema.
Hana muda mrefu kikosini na bado hajafahamu lugha vizuri, hivyo muda wake mwingi amekuwa anatumia kufanya mazoezi ili kukwepa upweke wa kuwa mwenyewe kutokana na kushindwa kupiga stori na wenzake changamoto ikiwa lugha.
“Anafanya sana mazoezi, hiyo ndio starehe yake akimaliza mazoezi ya pamoja akiona hana kitu cha kufanya huwa anarudi kufanya mazoezi ya ziada kwa upande wake mwenyewe,” anasema Walter.
KENNEDY MUSONDA-MCHUNGAJI, DJ
Ni mshambuliaji ambaye amedumu Yanga kwa msimu wa pili sasa akitokea Zambia, anapenda kuimba na kusali unaambiwa chumbani kwake huwezi kukosa biblia.
“Anapenda kusali, kuimba na ni mtu wa watu, mcheshi anapenda sana kwa sababu amekuwa akiamini kuwa muziki unampunguzia mawazo, unampa furaha,” anasema Walter na kuongeza;
“Wasanii wengi wa Tanzania anawakubali, lakini Harmonize ndiye amekuwa akimsikiliza sana na wimbo anaoupenda ni Yatapita aliomshirikisha Profesa Jay,” anasema.
Mahlatsi Makudubela maarufu kama Skudu, kiungo mshambuliaji anayemudu zaidi kucheza kama winga kutoka Afrika Kusini. Hapati namba sana kikosini na hatambi sana uwanjani kutokana na ubora wa wachezaji wanaocheza namba yake.
Hata hivyo, mashabiki wake wanampenda kutokana na vituko vyake kwenye uchezaji.
“Skudu anaweza asiwe bora, lakini akashangiliwa na mashabiki kwa vituko vyake, anapenda kuchezea mpira pia ni mtu ambaye anapenda kucheza muziki, hakuna muziki ambao haufahamu, kambini ni kama dansa flani kwa kucheza kila anaposikia muziki na hata ukiona tunapoingia uwanjani yeye anadansi,” anasema.