BENKI ya NMB imepandisha kiwango cha mikopo kwa wakulima na wafugaji kutoka Sh 730 bilioni mwaka 2021 hadi Sh 1.6 trilioni mwaka huu 2024 huku ikiweka mkakati wa kuinua sekta hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Kutolewa kwa mikopo hiyo kumesaidia kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji kwani kiasi cha Sh 505 bilioni ni mikopo ya wafugaji kwa lengo la kunenepesha mifugo na kuboresha maeneo ya malisho kwa kundi hilo.
Akizungumza mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan jana tarehe 8 Agosti 2024, Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna amesema kutolewa kwa mikopo hiyo ni sehemu ya mkakati wa benki katika kuunga mkono sera nzuri za Serikali ya awamu ya sita.
Takwimu hizo zimemfurahisha Rais Samia alipotembelea banda la maonyesho la NMB na kusema ‘Kazi Iendelee’ kauli ambayo huitumia anapokubaliana na jambo hasa kwenye miradi ya maendeleo.
“Rais tunakupongeza sana katika jitihada zako hasa ya kuwainua wakulima na wafugaji nchini, na sisi NMB tunayo mikakati ya kusaidia sekta ya kilimo na mifugo ambako tumeona kuna mapinduzi makubwa,” amesema Zaipuna.
Mtendaji Mkuu ameeleza kuwa kati ya mikopo iliyotolewa, Sh 450 bilioni zimetolewa kwenye mpango wa riba nafuu ya asilimia 9 ambako ndiko waliko wakulima na wafugaji.
Zaipuna amesema benki hiyo imeanzisha mkakati maalumu wa kuwafikia wakulima na wananchi kupitia mpango wake wa kufungua akaunti za Sh 1000 ambako mamilioni ya Watanzania wamejiunga huko hivyo kuwawezesha wananchi kupata mikopo kwa urahisi.
“Rais akaunti hii imerahisisha wananchi na wakulima kupata mikopo kwa njia ya mtandao (Mkopo fasta) bila kuweka foleni benki na mikopo hiyo inaanzia kiasi cha Shilingi 1000 hadi Shilingi milioni moja,” amesema.
Kiongozi huyo amemwambia Rais Samia kuwa benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kukuza maono na wametumia maonyesho ya wakulima Nane Nane kutoa elimu ya fedha ambako wananchi wamekuwa na mwitikio mkubwa.