Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ametoa wito kwa watanzania wenye sifa za kujiandikisha katika Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kujitokeza katika vituo ili kupata Kitambulisho cha Mpiga Kura kitakachowawezesha kupata haki ya kuchagua Viongozi katika Uchaguzi.
“Tukitaka kupata viongozi wazuri hatua ya kwanza ya kufanya ni kujiandikisha kwenye daftari ili tuweze kutumia haki yetu ya kidemokrasia muda utakapofika wa uchaguzi”, amesema Bashungwa.
Bashungwa ameipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuboresha zoezi hilo na kufanya kazi kwa weledi inayoimarisha Demokrasia nchini.
Aidha, Bashungwa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa kuendelea kuimarisha Demokrasia nchini na kuendelea kuiwezesha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.