Moshi. Vilio na simanzi vimetawala katika usharika wa Kisamo, Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), wakati wa kuaga mwili wa Mchungaji Kantate Munisi (42) ambaye atazikwa leo, usharikani hapo.
Wakati mwili wa mchungaji huyo ukiagwa kanisani hapo leo Agosti 09, 2024, mamia ya waombolezaji waliofika kushiriki ibada ya Maziko, walishindwa kujizuia kulia huku wengine wakianguka kutokana na kuishiwa nguvu.
Ibada hiyo ambayo imehudhuriwa na wachungaji kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo Dayosisi ya kaskazini alikokuwa akihudumu na Dodoma alikoanzia huduma, pia imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa taasisi za kanisa hilo na Serikali.
Mchungaji Munis ambaye alikuwa mchungaji kiongozi wa usharika wa Kimashuku, pamoja na Mzee wa usharika wa Kanisa hilo, Laban Kweka(50) walifariki dunia kwa ajali Agosti 4, 2024 baada ya gari walilokuwa wakisafiria wakitokea kwenye uimbaji wa Kanda usharika wa Gezaulole Wilayani Hai, kugongwa na basi la abiria.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro Agosti 5,2024, Simon Maigwa ajali hiyo ilitokea Jumapili Agosti 4,2024 katika eneo la Kimashuku, kata ya mnadani Wilaya ya Hai, mkoani humo, wakati mchungaji huyo akikatiza barabara upande wa kulia kuingia kanisani kwake na ndipo alipogongana na gari hilo.
Aidha, Kamanda Maigwa alisema dereva wa basi hilo amekamatwa kwa taratibu za kisheria, kwa kuwa alifanya uzembe kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari.
Endelea kufuatilia Mwananchi.