Karagwe. Mbunge wa zamani wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amesema Tanzania hakuna chama cha siasa kinachoweza kufanya kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo zaidi ya CCM, hivyo amewataka wananchi wasishawishike na wapinzani.
Msigwa ameeleza hayo leo kwenye mkutano wa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi uliofanyika katika Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku nne mkoani humo.
Mwanasiasa huyo alihamia CCM Juni 30, 2024 akitokea Chadema ambako amekuwa mbunge wa Iringa Mjini kupitia chama hicho kwa miaka 10 na mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa kwa miaka saba.
Mbali na kushika nafasi tofauti za uongozi, Msigwa amedumu kwenye upinzani kwa miaka 20. Hata hivyo, baada ya kushindwa uchaguzi wa Kanda ya Nyasa, alijiunga na CCM na kupokelewa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan alipotambulishwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
Akizungumza kwenye mkutano huo wa hadhara, Msigwa amesisitiza kwamba kwa uzoefu wake kwenye siasa, hajaona chama kinachoweza kuwaletea wananchi maendeleo zaidi ya CCM kwa kuwa kinajishughulisha na kero zao.
Amesema hospitali nyingi zimejengwa, vifaa tiba vimepelekwa. Amebainisha kuwa zamani baadhi ya vipimo vilikuwa vinafanyika Dar es Salaam pekee, lakini sasa watu hawalazimiki kwenda huko kwa sababu huduma hizo zinapatikana kwenye mikoa yao.
“Nasema kwa ujasiri mkubwa kwa kuwa nimekuwa kwenye upinzani kwa miaka 20…ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakipo chama kingine kinachoweza kufanya shughuli za maendeleo na kudumisha amani na utulivu.
“Kwa hiyo, mtembee kifua mbele kwamba Watanzania mko salama chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, chini ya CCM … msidanganyike kufanya kazi na upinzani,” amesema Msigwa kwenye mkutano huo.
Awali, mbunge wa Karagwe ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewahakikishia wananchi wa Karagwe kwamba Serikali imedhamiria kujenga barabara ya Karagwe – Kyerwa kwa kiwango cha lami na tayari mkandarasi amepatikana kwa ujenzi huo.
“Serikali inatambua changamoto ya barabara kwenye wilaya yetu, niwahakikishie kwamba barabara hizi zinakwenda kujengwa ili muweze kufanya biashara zenu za kahawa kwa urahisi zaidi,” amesema Bashungwa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Zainabu Katimba amesema takwimu zinaonyesha asilimia 22 ya wanafunzi wanaoanza shule hawamalizi, hivyo amewataka wazazi kuweka msisitizo kwa watoto wao.
“Tusimamie suala hili kama wazazi. Urithi pekee unaoweza kumwachia mtoto ni elimu. Tuhakikishe tunatimiza wajibu wetu wa kuwasaidia hawa watoto,” amesema Katimba.
Awali, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amesema huko nyuma kahawa ilikuwa inatoroshwa na kuuzwa Uganda lakini baada ya kuanzisha mfumo wa mnada, bei imepanda na sasa hakuna wanaokwenda kuuza nchi jirani ya Uganda.
“Rais Samia ameimarisha ushirikiano na mataifa mengine. Kyerwa na Karagwe mnapata umeme kutoka Uganda, haya ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya nchi zetu,” amesema Makalla.