Nguo, kovu vilivyowezesha mama kutambua mwili wa mwanawe uliookotwa ndani ya kiroba

Dodoma. Mwili wa mwanamke uliookotwa ukiwa ndani ya kiroba, umetambuliwa ikiwa ni siku 10 tangu ilipotolewa taarifa ya kupatikana kwake mkoani Dodoma.

Mwili huo uliokuwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma uliokotwa Julai 21, 2024 kwenye korongo katika Mtaa wa Chinyika, baada ya mkazi wa mtaa huo kuubaini alipokuwa akichunga mifugo.

Ulikuwa umefungwa kwenye nailoni na maboksi, kisha ukawekwa kwenye kiroba. 

Akizungumza na Mwananchi Mama wa marehemu huyo, Mary Msuya amesema aligundua mwili huo ni wa mwanawe Angela Stephano (23), aliyekuwa akiishi katika Mtaa wa Michese, Kata ya Mkonze usiku wa Julai 31, 2024.

Amesema alianza kuwa na hofu juu ya afya ya mwanawe baada ya kumpigia simu.

“Nilimpigia simu hakupokea lakini akanijibu kwa sms (ujumbe mfupi wa maneno) kuwa mama bwana tu-chat simu yangu ni mbovu. Nikamwandikia mtoto anaumwa akanitumia Sh25,000 ilikuwa ni Jumamosi (Julai 20, 2024),” amesema.

Amesema hawakuwasiliana tena na mwanawe ila alipata taarifa kupitia kwa mtoto wake mwingine anayeishi naye kuwa aliwasiliana na dada yake kwa njia ya sms akimtaka amtumie Sh50,000.

“Nikamwambia kwa hiyo unataka uibe vitu vya dukani kwangu umtumie dada yako fedha? Nikamwambia usichukue vitu vya dukani kwangu ukampa Angela yeye si ana maisha yake, akanijibu mama siwezi kufanya hivyo,” amesema.

Amesema siku zilivyoenda akajiuliza imekuwaje hakuna mawasiliano ya simu na mwanawe.

Mary amesema Julai 30, 2024 alifanya kazi ya kupika chakula cha kuuza kisha akeenda kwa mwanawe (Angela) aliyekuwa akiishi Michese.

Amesema alipofika aliuliza kuhusu mwanawe na kujibiwa na mama mwenye nyumba kuwa Angela hapatikani ila anafanya kazi kwenye duka la vipodozi.

“Akaniambia kuna kaka amekuja ametoa vitu vyote vya Angela hapo ndani. Nikamuomba namba za huyo aliyekuja kuchukua vitu, akanipa. Nilipompigia alipokea mwanamke nikamwambia kuwa namtafuta Jack maana nilishaambiwa jina la mtu aliyechukua vitu,” amesema.

Amesema dada huyo alimtukana matusi ya nguoni, jambo ambalo lilimfanya kukata simu baada ya kuona anadhalilishwa na mtoto mdogo.

“Huwa najiunganisha na maombi ya Mwamposa (Mchungaji) nikamwambia Mungu, naomba usiku nimpigie Angela nimpate. Kwa hiyo usiku nilipopiga nikamtafuta hapatikani, nikaendelea na maombi, roho ikaniambia rudi tena Michese,” amesema.

Amesema asubuhi (Julai 31, 2024) alienda tena kwenye nyumba aliyokuwa akiishi Angela lakini hakumpata mama mwenye nyumba, hivyo alimtafuta kijana anayefanya kazi katika kiwanda anakofanya biashara ya chakula.

Amesema baada ya kukutana na kijana huyo na kumtajia jina la mtu aliyechukua vitu vya mwanawe, alipatiwa namba nyingine ya simu ambayo alipoipiga ilipokewa tena na msichana huyo.

“Ilibidi tutumie mbinu kuwa tuna fedha za mtu aliyechukua vitu vya Angela kwa hiyo tunataka tukutane naye tumpatie fedha hizo. Tulikutana na dada yule tuliyekuwa tukiwasiliana naye, tulibaini simu aliyokuwa akitumia ni ya Angela,” amesema.

Amesema baada ya kubaini hilo, walimfuatilia ili kumkamata kijana huyo lakini hawakufanikiwa baada ya kuwadanganya eneo alipo, jambo ambalo lilimfanya kumpeleka msichana huyo polisi na kutoa maelezo juu ya mwanawe kutoonekana.

“Nikatoa maelezo kwa polisi ambao walisema kuna binti aliokotwa Michese na kuwa niangalie nguo kama nitazifahamu, wakatoa boksi na nguo kuangalia kwanza lile boksi tu nikalijua. Wakaleta kamera wakanionyesha picha nikawaeleza huyo mtoto ni wa kwangu,” amesema.

Amesema usiku wa siku hiyo, laini ya Angela ilikuwa hewani na alitumiwa sms kuwa asiwe na hofu kwa kuwa yupo Dar es Salaam amepata kazi ya kuuza duka la vipodozi na kuwa baada ya muda simu yake itakuwa hewani.

Amesema kesho yake asubuhi alikwenda mochwari ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma alikoonyeshwa mwili wa mwanawe ambao hakuweza kuutambua kirahisi hadi alipoona kovu lililotokana na kuumia tangu alipokuwa mdogo.

Mama huyo alipoulizwa iwapo mwanawe alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na kijana huyo, amesema hawezi kufahamu kwa kuwa hajawahi kutambulishwa.

Amesema mtoto huyo alizikwa Agosti Mosi, 2024 Babati mkoani Manyara.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya akizungumza na Mwananchi leo Agosti 9, 2024 amethibitisha mama huyo kuutambua mwili huo.

“Baadhi ya watuhumiwa wamekamatwa lakini mhusika bado tunamtafuta,” amesema.

Related Posts