Nangaa na washtakiwa wengine 15 walishtakiwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita, kushiriki katika vuguvugu la uasi na uhaini.
Jaji wa mahakama hiyo ya kijeshi ya Kinshasa Gombe Kanali Efomi Lonteyandjoko Jean-Robert, ndiye aliyetangaza hukumu hiyo dhidi ya washitakiwa Corneille Nangaa pamoja na wafuasi wake.
Waendesha mashtaka kutofurahia faini
Akizungumza na wanahabari baada ya wateja wake wote kuhukumiwa kifo, mwanasheria Peter Ngomo alisema, kwamba kuna baadhi ya wateja wake waliohukumiwa bila ya makosa yao kuhakikishwa na mwendesha mashtaka.
Mfano mmoja, ni hukumu dhidi ya Nangaa Baseane Putters, mjomba wa kiongozi wa waasi AFC-M23 Corneille Nangaa.
“Hapo tunachanganywa, kwani mwendesha mashataka hakumshtaki mteja wangu kwa ajili ya uhaini, lakini mahakama inamuhukumu kwa kosa la uhaini. Sijaelewa vizuri. Wanamuhukumu kwaajili ya kujiunga na kundi la uasi, sasa alifanya kosa gani isipokuwa ile ya jina lake kuitwa tu Nangaa? Kwangu mimi hakuna vithibitisho kwamba ni muasi. Kesho tutakata tufaa,” alisema Peter Ngomo.
Pamoja na kwamba wanasheria wa upande wa mashtaka walifurahia hukumu iliyotolewa na majaji dhidi ya watuhumiwa, lakini hawakukubaliana na faini wanaotakiwa kulipa wahukumiwa.
Mwanasheria Dolly Mwanza anasema, kuwa dola bilioni moja za fidia hazitoshi na angependa kitita zaidi.
“Nitasema kwamba kitita cha dola za kimarekani bilioni moja hakitoshi, kutokana na madhara yaliyosababishwa na uasi wa Nangaa,” alisema Dolly Mwanza.
Wanaharakati waelezea wasiwasi kuhusu hukumu ya kifo
Kesi ikiwa inafanyika baada ya serikali ya Congo kuamua kuwanyonga watu waliohukumiwa kifo. Wziri wa Sheria Constant Mutamba amesema, kwamba atahakikisha hukumu hiyo inatekelezwa, ilikuwaonya wale walio na nia ya kuisaliti nchi.
“Nitafuatilia mwenyewe, nakufanya juu chini, hasa baada ya muda wa kukata rufaa kumalizika na wakati hukumu itaanza kufanya kazi, ili hukumu ya kifo itekelezwe kwa matendo. Hilo litakuwa somo kwa wale ambao watajaribu tena kuisaliti nchi,” alisema Constant Mutamba.
Hata hivyo wanaharakati wa haki za binaadamu wameonyesha wasiwasi kuhusu utekelezaji wa hukumu ya kifo, wakihofia serikali kutumia fursa hiyo kuwaua wapinzani, kama anavyosema mwanasheria Justin Matete, wa shirika Forum de Paix.
“Hofu yetu nikuona siasa inaingilia kati. Hatujapinga hukumu iliyotangazwa, bali tunawaomba watu kufungua macho, ili isiwe nafasi ya watu kulipizana kisasi,” alisema Justin Matete.
Akipinga hukumu dhidi yake, Adam Chalwe, mmoja wa wahukumiwa na anaeishi katika wilaya ya Rutshuru alisema kupitia ukurasa wake wa X, kwamba hapa na munukuu, “hukumu dhidi yetu inayotokana na ukombozi wa nchi ni kama nyota inayoangaza na ni alama ya uzalendo wetu”, mwisho wa kumunukuu.
Wahukumiwa wanazo siku tano ili kukata rufaa.