BAADA ya kutoa asisti ya bao pekee katika derby Yanga na Simba Juzi mechi ya pili ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii, mshambuliaji mpya wa kikosi hicho Prince Dube amefunguka kuwa haamini kama hakutikisa nyavu mbele ya Wekundu hao.
Dube ambaye alisajiliwa dirisha hili akitokea Azam FC, ni miongoni mwa washambuliaji wanaosifika kwa kuisumbua Simba pindi inapokutana na timu wanazochezea.
Rekodi zinaonyesha mchezo wa mwisho aliitungua Simba bao moja katika mechi ya Dabi ya Mzizima katika Uwanja wa CCM Kirumba.
Akizungumza na Mwanaspoti baada ya mechi hiyo Dube alisema, mpaka sasa haamini mechi dhidi ya Simba imekwisha na ametoka bila kuwafunga.
Aidha alisema shambulizi la kipindi cha kwanza lililogonga mwamba aliamini kwamba mpira umeingia ndani ndio maana alishtuka kuona haujaingia wavuni.
“Nilipanga kuendeleza rekodi yangu ya kuwa nyoosha Simba ijap haikufanikiwa ila nilipambana sana kuifunga hata lile shuti ambalo halikuwa bao lilionyesha jinsi gani nilivyotamani kutumia nafasi.
Lakini nimefurahi kwani nimeshiriki kutoa asisti ya bao pekee ambalo limeivusha tim yetu kwenda fainali na Mungu ajalie tuwe Mabingwa,” alisema Dube.
Staa huyo kwa mara ya kwanza Agosti 11 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa atakutana na kikosi chake cha zamani katika fainali ya Ngao ya Jamii.