Waokota chupa za plastiki wakatiwa bima ya afya

Dar es Salaam. Wazalishaji wa vinywaji na watengenezaji wa bidhaa za plastiki nchini, wamewapatia waokota chupa za plastiki bima ya afya ya jamii (CHF) na viakisi mwanga vyenye namba kutokana na kuwa na mazingira hatarishi ya ufanyaji kazi zao.

Katika kutambua mchango wa waokota chupa   hao wazalishaji wa  vinywaji nchini kwa kushirikiana na taasisi zinazojihusisha na ukusanyaji wa chupa  na mtandao wa ajira zisizo rasmi wametoa bima za afya na kiakisi mwanga kwa vijana 50.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumamosi Aprili 27, 2024 Mratibu wa taasisi ya urejereshi nchi (PETpro), Nicholaus Ambwene amesema lengo la kuwapa bima hiyo waokota chupa za plastiki ni kuwalinda na hatari zote wanazokumbana nazo wanapokuwa kwenye majukumu yao, kwani wamekuwa watu muhimu katika kuhifadhi mazingira.

“Hawa watu wanafanya kazi muhimu katika nchi yetu ni vile tu hawathaminiwi na kuheshimika kutokana na mwonekano wao, kwani bila ya uwepo wa hawa watu hali ya mji sijui ingekuaje kwenye utupaji wa chupa,” amesema Ambwene.

Amesema uzalishwaji wa chupa za plastiki ni mkubwa lakini urejeshwaji wake umekuwa na changamoto, hususani kwenye chupa za rangi ambazo waokotaji hawazichukui kutokana na gharama yake kuwa ndogo.

Nicholaus amesema kuna kampuni zinazalisha tani 200 kwenye soko na hajui ni namna gani anaweza kuzirejesha ili kulinda mazingira, lakini wanaookota chupa hizo wamerahisisha kuifanya kazi hiyo kuwa nyepesi.

“Kuna chupa ambazo hazichukuliwi na ndizo zinazoonekana kuzagaa hata kwenye vyanzo vya maji kutokana na gharama yake kuwa ndogo ambayo kilo ni Sh100, hivyo kwa kushirikiana na kampuni zinazozalisha chupa za rangi tumeongeza gharama kilo itakuwa Sh200,” amesema Ambwene.

Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ally Mtumbuka amesema, “kama zinajitokeza kampuni na kuthamini wazoa taka kwa kuwapatia vifaa na bima ya afya kuna haja ya jamii kuthamini mchango wa watu hao katika kutunza mazingira wilayani humo na Taifa kwa ujumla,” amesema Mtumbuka.

Pia, ametoa ushauri kwa taasisi zinazojihusisha na mazingira kujitanua zaidi kufikia zote  36 za wilaya ya Ilala na ikiwapendeza wanaweza kwenda hadi pembezoni mwa mjini ikiwepo maeneo ya Chanika na Zingiziwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ukusanyaji taka ya Juza, Nassib Kitabu amesema amekuwa na vijana 600 wanaokusanya chupa mtaani katika kata ya Jangwani na Mchafukoge, hivyo kupatikana bima ya afya na viakisi mwanga itawasaidia kwenye shughuli zao.

Juma Kaombwe mwokota chupa amesema wamekuwa wakikutana na changamoto nyingi ikiwamo  kusingiziwa wizi kwa kuwa hawana utambulisho maalumu kama ilivyo kwa wafanyabiashara wengine.

“Waokota chupa tupo wa aina mbili tuliodhamiria kujiingizia kipato kupitia chupa na wanaoingia kwenye nyumba za watu kwa lengo la kuiba, hivyo kupewa vifaa na bima ya afya itatutofautisha kwa kuwa tutakuwa tunatambulika kwa namba,” amesema Kaombwe.

Asha Zuberi, mkazi wa Kariakoo amesema kilichofanyika ni kizuri kwa kuwa kitasaidia kuwatambua wahalifu katika maeneo yao na taarifa zitafika kwa mtu anayewasimamia.

Related Posts