JESHI la Polisi mkoa wa Katavi limewakamata watuhumiwa wawili wa mauaji ya dereva bodaboda ambaye anadaiwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali ubavu wa kushoto na mwili wake kutelekezwa barabarani kisha watuhumiwa kutokomea na pikipiki yake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Katavi … (endelea).
Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, SACP- Kaster Ngonyani amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Japhet Pangani Didas, (32) Mkazi wa Wilaya ya Nkasi mkoa wa Rukwa na Shaban Said Maelezo (64) mkazi wa Urumi Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa.
Amesema watuhumiwa hao wamehusika katika tukio la mauaji ambapo tarehe 24 Julai 2024 saa 07:00 usiku katika kitongoji cha Kiloleni kijiji cha Sitalike Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi walimuua Michael Geofrey Mkuyu, (23) Dereva pikipiki (bodaboda) Mkazi wa Makanyagio Mpanda.
“Watuhumiwa hao wanadaiwa kumchoma na ktu chenye ncha kali maeneo ya ubavuni wa kushoto na kulia na kisha mwili wake kuutelekeza pembezoni mwa barabara na kisha kuondoka na pikipiki yake yenye namba za usajili MC 163 CKC aina ya Boxer.
“Baada ya kutendeka tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi lilianza msako mkali na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.
Walipohojiwa walikwenda kuonyesha walipouza pikipiki waliyompora Michael Geofrey Mkuyu baada ya kumuua,” amesema.
Aidha, amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi linawaasa wananchi kuacha tabia ya tamaa ya kutamani mali ya mtu mwingine mpaka kufika hatua ya kutoa uhai wake, kwani watasakwa popote pale watakapo kimbilia ili hatua kali na za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.