HATIMAYE Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeibuka na kutoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa za mahali alipo kijana Shadrack Chaula (24) Mkazi wa Kijiji cha Ntokela Wilayani Rungwe mkoani Mbeya aziwasilishe kwa jeshi hilo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mbeya … (endelea).
Hatua hiyo imejiri baada ya tarehe 2 Agosti mwaka huu baba mzazi wa kijana huyo, Yusuph Chaula (56), kutoa taarifa za kutoweka kwa mwanaye huyo ambaye alinusurika kifungo cha miaka miwili gerezani kwa kosa la kuchoma picha ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Tarehe 10 Julai kijana huyo aliachiwa huru kutoka mikononi mwa jeshi la magereza baada ya kufanikiwa kulipa faini ya Sh tano milioni kutokana na Mahakama ya Wilaya ya Rungwe kumkuta na hatia ya udanganyifu.
Hata hivyo, baada ya kutoweka, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mbeya, SACP – Benjamin Kuzaga ametoa wito kwa mwenye taarifa zake kijana huyo aziwasilishe kwa njia iliyosahihi kwa viongozi wa Jeshi la Polisi ili kufanikisha kuwapata watu waliomchukua kijana huyo, lakini pia linaendelea kufanya uchunguzi wa kina na litatoa taarita kwa umma.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda Kuzaga jana Alhamisi imesema Jeshi la Polisi lilipokea taarifa za kutoweka nyumbani kwao kijana huyo tarehe 2 Agosti 2024 majira ya saa 8:30 mchana kutoka kwa baba mzazi wa kijana huyo aitwaye Yusuph Chaula [56] Mkazi wa Ntokela.
Amesema jeshi hilo limeanza kufanya ufuatiliaji na uchunguzi kuhusu taarita hizo, hivyo linawataka wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki linapoendelea na uchunguzi.
“Aidha, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa za mahali alipo kijana huyo aziwasilishe kwa njia iliyosahihi kwa viongozi wa Jeshi la Polisi ili kufanikisha kuwapata watu waliomchukua kijana huyo, lakini pia linaendelea kufanya uchunguzi wa kina na litatoa taarita kwa umma,” amesema.