Arusha/Dar. Watafiti wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) wamegundua dawa ya kutibu ugonjwa wa malaria isiyo na kemikali.
Wataalamu hao kwa kushirikiana na watafiti kutoka taasisi zingine za tiba nchini Kenya (KEMR) na Afrika Kusini wamegundua dawa hiyo mwishoni mwa Julai, 2024 baada ya utafiti wa kina wa miaka mitatu.
Dawa hiyo inaelezwa ni ya kwanza ya ugonjwa wa malaria kupatikana Afrika, nchini Tanzania iliyopewa jina la ‘Plasquin’. Inakuwa ya pili duniani baada ya R21 iliyotengenezwa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Oxford na Burkina Faso na kutangazwa na Shirika la Uzalishaji wa Chanjo duniani Gavi Alliance mapema mwaka jana.
Ugunduzi wa dawa hiyo umefanyika wakati ambao idadi ya wanaobainika kuwa na ugonjwa wa malaria imeongezeka.
Akizungumza Aprili 30, 2024 alipofungua kongamano la malaria kwa mwaka 2024, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu alisema wagonjwa wa malaria wametajwa kuongezeka kwa kipindi cha mwaka 2023.
Takwimu zinaonyesha Zanzibar mwaka 2022 waliripotiwa wagonjwa 4,000 wa malaria, lakini mwaka 2023 kulikuwa na ongezeko kufikia wagonjwa 19,000, huku asilimia 80 kati yao wakitokea Mkoa wa Mjini Magharibi.
Tanzania Bara takwimu zinaonyesha mwaka 2022 kulikuwa na wagonjwa 3,478,875 na mwaka 2023 walikuwa 3,534,523 sawa na ongezeko la asilimia 1.6, huku vifo vikiongezeka kutoka 1,430 mpaka 1,954 mwaka 2023.
Akizungumza leo Agosti 9, 2024 jijini Arusha kwenye maonyesho ya wakulima maarufu Nanenane, Kanda ya Kaskazini, mtafiti wa masuala ya tiba kutoka Taasisi ya NM-AIST, Dk Daniel Shadrack amesema dawa imepatikana kutokana na utafiti wa kina wa miti shamba inayotumiwa kama tiba ya asili ya ugojwa wa malaria.
“Mara nyingi tiba hii ya asili ilihusisha miti shamba aina tofauti ikiwemo mti wa ‘Sindelela Ondorata’ baada ya utafiti tuligundua kweli ina uwezo mkubwa wa kutibu na kukinga ugonjwa wa malaria,” amesema Dk Shadrack na kuongeza:
“Baada ya kuona hivyo tulianza utafiti wa kuiweka katika viwango vitakavyokubalika kwa njia ya vidoge, tumefanikiwa na sasa tunatarajia itakuwa msaada mkubwa kwa nchi za Afrika katika vita dhidi ya malaria,” amesema.
Kuhusu chanjo ya malaria, Dk Shadrack alisema, “bado hatujapiga hatua kubwa katika mchakato wake, isipokuwa dawa ya malaria tumefika mbali ambayo ina uwezo wa kutibu na kukinga.”
“Mchakato wa kutengeneza dawa umepiga hatua kubwa zaidi huu ni mwaka wa tatu, tunaendelea na utaratibu wake, lakini angalau sasa tuna vidonge tayari vinavyofanyiwa kazi. Hatua inayofuata ni majaribio kwa binadamu ambapo siwezi kutamka kwa sasa itakuwa ni mwezi gani,” amesema Dk Shadrack.
Amesema muda si mrefu wataanza hatua ya majaribio ya dawa hiyo, ingawa kuna baadhi waliotumia ikatibu malaria ambao wamekuwa wakimeza vidonge viwili kila baada ya saa tatu.
Amesema majaribio yakifanyika hospitalini yatatoa majibu kuhusu matumizi ya dawa hiyo kwamba mtu atumie vipi na kwa muda gani.
“Tofauti ya dawa hii na zile zinazotengenezwa nje ya nchi, ni kwamba imetengenezwa kiasili zaidi kwa kutumia miti yetu ingawa ipo katika vidonge na haina madhara, ufanisi wake ni mkubwa,” amesema.
Makamu Mkuu wa Taasisi ya NM-AIST, Profesa Maulilio Kipanyula amesema wanatarajia kuiwasilisha kwa mamlaka za dawa na tiba kwa ajili ya kuithibitisha.
“Dawa hii iliyotokana na miti shamba tunatumai itakuwa ngao njema dhidi ya malaria na kuokoa maelfu ya watu wanaokufa kutokana na ugonjwa huo barani Afrika na dunia kwa ujumla,” amesema.
Akizungumza katika maonyesho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amewataka watafiti hao kuharakisha mchakato wa uthibitishwaji wa dawa hiyo itakayokuwa msaada kwa watu wanaougua malaria.