Utekaji watoto: Marejeo ya ‘Jini Mbuzi’?

Dar es Salaam, Elimu ni ufunguo wa maisha wa jamii yoyote chini ya jua. Zamani Watanzania wengi hawakuwa na Elimu ya kutosha, kilichosababisha Taifa letu kuzorota kiuchumi na kimaendeleo.

Bila elimu mtu angeshindwa kupanga maisha yake kwani asingeweza kusoma vipeperushi vya afya na hata kupanga hesabu za mapato na matumizi yake. Wangekosa ajira na wakulima wasingeweza kwenda na kilimo cha kisasa. 

Wakati ule ukitaka kumtukana mtoto wa mjini mwite “mkulima” au “mshamba”. Hili lilitokana na watu wasio na elimu kukosa ajira za mijini na kukimbilia kwenye kilimo mashambani.

Hali hii ilipelekea uongozi wa Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Nyerere kuzindua mpango wa Elimu ya Watu Wazima (ngumbaru) na baadaye Elimu kwa Wote (UPE) mwishoni mwa miaka ya sabini.

Lakini kama kawaida hakuna mchele unaokosa chuya. Kwenye maendeleo kama hayo ni lazima patokee watu watakaoharibu ili wajenge fursa. Uwazi kuna walozi wanaojifanya waganga, wanaitia maradhi jamii yao kisha kuvaa shuka za waganga na kupiga ramli. Hiyo ndiyo njia yao pekee ya kupata maokoto kwani kila mtu akierevuka watashindwa kutia mkono kwenye kapu la mjanja.

Enzi zile kwenye mpango wa Elimu kwa Wote kuliibuliwa taharuki ya “Jini Mbuzi”. Wahuni waliiona fursa kwenye ongezeko la Shule za Msingi. Inawezekana wahuni hawa walikuwa ni wale waliokimbia umande wakawaacha wenzao wakipanda vidato hadi kuwa walimu wakuu wa shule tulizosoma. Kwa vile utotoni mwao walicheza chandimu pamoja na walimu wetu, wakaona “hawa mbona tunawaweza?”

Basi wakatengeneza mpango kazi wao na kuanzisha taharuki ya Jini Mbuzi. Kwenye Shule moja walimwachia mbuzi aliyevalishwa kanzu na balaghashia, na kwenye shule zingine walivamia madarasani wakiwa wamejifunika mashuka meupe.

Jambo hili lilisababisha watoto kuzikimbia shule na wazazi wakagoma kuwarudisha hadi jini huyo atakapodhibitiwa.

Wahuni si watu wazuri. Wakaanza kuwafuata walimu majumbani mwao na kudai kuwa hata huko vijijini wanakotoka kulikumbwa na dhahama kama hiyo, lakini waliidhibiti baada ya kuwaita waganga kutoka Kongo na Msumbiji.

Waliendelea kudai kuwa waganga hao wangalipo hapa nchini wakimalizia kazi katika kanda zingine. Walimu wetu wakauingia mkenge na kuwapa wahuni pesa za kufanya koneksheni na waganga.

Wahuni wakawaleta wahuni wenzao na kuanza kufukiza ubani pale shuleni. Na kweli tatizo likaisha kwani lilimalizwa na waliolianzisha. Lakini kwenye shule ambazo walimu wake walikataa kumwaga maokoto, hali ikazidi kuwa mbaya. Hata hivyo sisi tuliathirika sana kisaikolojia kwani sote tulipoteza tafakari za darasani.

Muda wote tuliketi tukikodoa macho huku na huko. Alipoonekana mbuzi wa Mwalimu Mkuu sote tulikula kona!
Hivi karibuni imezuka hofu ya watoto kutekwa mashuleni. Hofu hii imeongezeka baada ya taarifa za baadhi ya watoto kuuawa na kukatwa viungo vya miili yao. Wazazi wamekosa amani kiasi cha kuchelea kuwatuma watoto sokoni kama wanavyochelea kuwaachia waende shuleni.

Hali inazidi kuwa ngumu pale mzazi anapolazimika kuchagua moja kati ya kubaki nyumbani akilinda watoto au kwenda kazini kutafuta fedha ya kuwakimu watoto hao.

Hivi majuzi mzazi msamaria mwema alikoswa kukatwa masikio na wazazi wenye hasira kali baada ya msamaria huyo kuwapa lifti rafiki za mwanaye wanayesoma naye. Mashuhuda waliona gari ndogo ikipakia watoto zaidi ya watatu, habari zikarushwa mtandaoni na sekunde hiyohiyo wazazi wakawa wamemzunguka.

Kwa maelezo yake, msamaria huyo alisema kwamba alitaka kuwasaidia watoto wale kwa vile waliishi mitaa ya jirani na kwake.

Lakini pamoja na habari za uhakika za kukatwa viungo kwa watoto hasa walemavu wa ngozi, kumekuwa na uzushi wa kimtandao unaowapeleka mbio wazazi. Ghafla tu tetesi zinasambaa “Watoto wanatekwa kwenye Shule ya Msingi Nanihii…”.

Hapo kila mzazi mwenye mtoto katika shule hiyo hana budi kwenda kasi kuhakikisha usalama wa mtoto wake. Imeshuhudiwa mara kadhaa wazazi wakiandamana shuleni wakidai kuoneshwa watoto wao.

Hatujajua nini hasa lengo la watu wanaozua taharuki. Tishio lililopo si la uzushi kwani mpaka sasa kuna ushahidi wa watoto waliopatikana baada ya kuibwa, na zipo taarifa za wengine ambao hawajapatikana. Kama wazushaji wanafanya hivyo wakitegemea kupata maokoto, haijaeleweka wanayatega kivipi. Bora wenzao wa Jini Mbuzi waliotufumba macho kwa muda fulani wakivuta michuzi kutoka kwa walimu.

Wote hawa (wanaopoka watoto na wapotoshaji wa taarifa) wanawayumbisha watoto kielimu. Mtoto hawezi kusimamia masomo yake anapokuwa kwenye wasiwasi wa kutekwa. Hasara tuliyoipata sisi tuliomkimbia Jini Mbuzi ndiyo wanayoipata wanaomkimbia mteka watoto. 

Ninaamini Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi litaongeza ulinzi kwa watoto. Pia naamini kuwa linaweza kufanya ukachero na kuwanasa wapokaji wa watoto mmoja baada ya mwingine. Vilevile natumai litafanya juu chini kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kuwanasa wapotoshaji wa taarifa za matukio hayo. Hawa nao wana umuhimu wa kufikishwa mbele ya sheria kujibu madhambi yao.

Related Posts