Dk Biteko atoa maagizo kilio cha kodi, tozo shule binafsi

Dar es Salaam. Kufuatia kilio cha utiriri wa tozo kwa shule binafsi nchini, Serikali imeagiza wizara tano kukutana na Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi Tanzania (Tapie) kutafutia ufumbuzi kero zinazolalamikiwa.

Serikali imetoa tamko hili ukiwa ni mwezi mmoja kupita tangu gazeti hili kuandika kilio cha wadau hao kwenye kodi wakidai zipo takribani 25 zinazowanyima usingizi.

Baadhi ya kodi hizo ni inayokatwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Usalama Mahala pa Kazi (Osha), halmashauri kodi ya ardhi, viwanja vya michezo ambavyo wanafunzi wanachezea mpira.

 Baada ya  kilio hicho kwa Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko alimuelekeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama kuandaa mkutano utakaohusisha Wizara ya Fedha, Wizara ya Ardhi Maendeleo ya Makazi,

 Ofisi ya Rais Tamisemi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na wizara inayoshughulikia uwekezaji kujibu kero za wadau hao.

Jana, akifungua, mkutano wa tano wa Tapie jijini Dar es Salaam, Dk Biteko alilazimika kutoa maagizo hayo baada ya hotuba iliyowasilishwa kwake na Rais wa chama hico, Dk Mahmoud Mringo akiomba Serikali kuondoa kodi na tozo zinazochangia gharama ya elimu kupanda.

“Kodi zikiondolewa zitaleta tija zifuatazo, kupunguza gharama za utoaji wa elimu na hivyo ada ya shule kuwa nafuu, kuipunguzia Serikali mzigo wa ujenzi wa miundombinu msongamano shule za umma, na kuwekeza zaidi katika uimarishaji wa ubora wa elimu na masilahi ya wafanyakazi,” amesema.

Dk Mringo amesema Serikali inawatoza tozo hata kwenye viwanja ambavyo wamevitenga kwa ajili ya michezo ya watoto jambo waliloliona hakuna haja tena ya wanafunzi kucheza shule, bali wavipime viwanja hivyo na kuvipiga mnada.

Katika maelekezo yake, Dk Biteko amesema ni muhimu watu waambiwe ukweli yale yanayowezekana waambiwe na yasiyowezekana waambiwe pia.

“Yapo mambo yanayowekezana, hayo sitaki niseme na yapo ambayo hayawekezani, kwamba sasa hii kodi niachie haiwezekani si kodi zote zinazokusanywa zinapaswa kwenda kwenye elimu hapana, kuna miradi mbalimbali ya nchi tunahitaji fedha na Serikali haichapishi fedha inazalisha kupitia kodi.”

“Sekta binafsi mnapaswa kujivunia kulipa kodi, sasa kodi kuongeza gharama za ada ni suala la kiuchumi, zipo tozo zinazogusa ardhi inayotumika kwa matumizi ya jamii mtajadili na kupata majibu,” amesema Dk Biteko.

 Ili kupatiwa ufumbuzi endelevu wa changamoto zinazowakabili, Dk Biteko amekiagiza chama hicho kuwasilisha serikalini wakati wote mawazo waliyonayo na Serikali itawaita na kuyajadili.

 Akifafanua zaidi, Dk Biteko amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan haiwezi kuwaacha wawekezaji hao waendelee kulalamika.

Hoja ya kupunguzwa kwa tozo inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko akisema  Serikali inapaswa kuziangalia upya tozo zilizopo. “Suala la tozo, leseni za kuanzisha shule Serikali inapaswa kukaa na wadau halmashauri kuziondoa,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dk Biteko amewaagiza wamiliki wa shule kuacha tabia ya kuwafukuza wanafunzi wanaopata alama ndogo, baada ya kufanya mtihani.

 Dk Biteko amesema kumfukuza mwanafunzi ambaye hakuwa na alama nzuri darasani ni ishara ya wahusika kutotimiza wajibu wao.

 Jambo lingine aliloagiza Dk Biteko ni Tapie kuimarisha malezi bora kwa watoto, kusimamia masharti ya usajili wa shule hizo, kuwasilisha serikalini maoni na mapendekezo waliyonayo kuhusu sekta ya elimu pamoja na kuajiri walimu wenye sifa.

“Wanafukuza kwa sababu ya alama ndogo, tunataka kuchagua watoto wenye uwezo tukae nao, ukimuondoa mwanafunzi shuleni kwa sababu hakufikisha alama fulani na wewe hukutimiza wajibu wako,” amesema.

Agizo la pili la Dk Biteko ni chama hicho kusimamia suala la maadili, kwani wanafunzi wanaozalishwa kwenye shule binafsi hawawezi kujitegemea (maofisa).

“Badala ya kuzalisha watu wa kujitegemea anakuwa mtegemezi wa kila kitu, akidondosha kalamu anataka aokotewe anakuwa ‘bumunda’ tu, lakini ukimwambia azungumze anaongea balaa, akiwa mtu mzima hajui kufua, kupika sasa lazima muandae watu wa kujisimamia wenyewe,” amesema.

 Kufuatia hoja wanafunzi kukosa maarifa, Katibu Mtendaji wa Taasisi inayojishughulisha na masuala ya elimu Everon Hope Foundation, Said Juma amesema hiyo  inatokana na shule nyingi kuwapo kibiashara.

“Wamejikita zaidi kwenye nadharia ndio maana shule nyingi hazina maabara, kwa hiyo Serikali ingeweka utaratibu wanafunzi wawe wanafundishwa na kutenda,”amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akijibu hoja ya hitaji la sheria mpya ya elimu aliwataka wadau hao kufanyia mapitio na kueleza mambo yanayohitaji mabadiliko. “Tutakwenda kwa mwanasheria mkuu wa Serikali atatuambia ni marekebisho madogo au ya namna gani yatahitajika ninavyohisi itahitajika sheria mpya, lakini ninyi ndio mtaamua,” alisema.

Katika kuunga mkono juhudi za kuboresha elimu nchini, Benki ya CRDB ilisaini mkataba wa ushirikiano na Tapie utakaowawezesha wanachama wake kupata mikopo nafuu ya kuboresha miundombinu na kuwezesha uendeshaji wakati wote.

Ofisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo amesema  wanatambua  changamoto wanazokutana nazo wamiliki binafsi wa shule, hivyo imechukua hatua za kusaidia kuzitatua ili kuwa na mazingira rafiki kwa wanafunzi kusoma na kujifunza.

Related Posts

en English sw Swahili