Watanzania hutumia miaka 10 hadi 15 kujenga nyumba

Dar es Salaam. Licha ya kuwepo kwa mwamko wa wananchi kujenga nyumba kupitia fedha zao za mfukoni, hali inaonyesha kuwa huwachukua wastani wa miaka kumi  hadi miaka 15 kumaliza kujenga nyumba hizo.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Agosti 9,2024 na Mkurugenzi Mkuu  wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah, alipokuwa akitoa  taarifa ya shughuli zinazofanywa na Shirika hilo kwa  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, alipotembelea shirika hilo, ikiwa ni  mara ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.

Abdallah amesema ni kutokana na hilo, Shirika limekuwa likifanya kila liwezalo katika kuwasaidia kuifanya kazi hiyo, licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika kuzitimiza ndoto hizo.

“Mpaka sasa asilimia 99 ya Watanzania wanajenga nyumba kupitia fedha za mfukoni mwao ambazo nyingi ni zile za kudunduliza na hivyo kuchukua muda mrefu kuzimaliza,’’ amesema.

Ni kutokana na hilo amesema wengi wao huishi katika nyumba ambazo bado hazijamalizika na pale wanapopata fedha, humalizia chumba kimoja kimoja wakiwa ndani.

Pia Abdallah amesema takwimu pia zinaonyesha mpaka sasa  kuna uhaba wa nyumba milioni 3.8 huku uhitaji wa nyumba kila mwaka ukiwa ni 3000 na kati ya nyumba hizo zipo za kupanga au za kununua.

“Ukiangalia kwa kazi tunayoifanya tunatakiwa kupambana na uhitaji wa watu wa nyumba hizo lakini wakati huohuo kuangalia ongezeko la watu na kuitumia kama fursa katika biashara ya nyumba.

“Takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufika mwaka 2050, asilimia 44 ya Watanzania watakuwa wanaishi mjini na hali hiyo imeanza kujionyesha namna Dar es Salaam kwa sasa ilivyojaa na wengi huishi mkoani Pwani na kuja kufanya kazi Dar es Salaam.

“Vilevile kuanza kwa mradi wa treni ya umeme tutegemee watu wengi wataishi Morogoro na kuja kazini Dar es Salaam,” amesema Abdallah.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndegembi (katikati) akizungumza na Menejimenti ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) alipofanya ziara katika ofisi za shirika hilo jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake,  Waziri Ndejembi amesema pamoja na maono hayo ya shirika ni vema kukajengwa nyumba si tu za bei rahisi kwa wananchi wa vipato vya chini, lakini pia ziwe katika maeneo yanayofikika kirahisi ili kuwapunguzia gharama ya maisha ikiwemo usafiri.

Pia amesema wanaangalia namna gani mtu mwenye nia ya kununua nyumba za NHC akiwa ameshalipia asilimia 10 hadi 20, iliyobaki atalipa kodi kama mpangaji kwa miaka kadhaa mpaka fedha yake itakapokamilika kisha kumilikishwa rasmi.

“Hili tutakaa na menejimenti kuona ni namna gani nzuri katika kulifanya hili, lengo likiwa kuwawezesha Watanzania wengi kumiliki nyumba zao,” amesema Waziri huyo.

Mkazi, Martha Chiluba, amesema bado kuna kazi ya ziada ya kufanywa na shirika hilo kama limedhamiria kila Mtanzania kuwa na nyumba ikiwemo kupunguza bei za nyumba zake.

“Kila wakati tunasikia wakitangaza nyumba zao ambazo za watu wa kipato cha chini zinaanzia Sh50 milioni kuendelea kwa maisha yetu, hela hizo kuzipata ni ngumu ndio maana mtu anaona ajenge chumba chake kimoja au viwili aingie kuepuka kodi, ‘’ amesema Martha.

Ivan Kajiru, amesema ifike mahali kuwe na ukomo katika kupangisha nyumba za shirika hilo, kwani kuna ambao wamefanya kama mali yao na vizazi vya kurithishana na kuna baadhi tangu miaka ya 1970 wanakalia nyumba hizo jambo ambalo sio sawa.

Mpaka sasa NHC ina majengo 2,872 yenye sehemu za kupangisha zipatazo 20,349 ambapo sehemu ya nyumba 1,540 ni za wamiliki wa awali (ex-owners).

Pia Shirika hilo lina sehemu za kupangisha zipatazo 17,916 ambapo sehemu za biashara ni 7,202 na sehemu za makazi ni 10,714.

Hata hivyo ndani ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Shirika hilo limepanga kujenga nyumba 5000, kati ya hizo asilimia 50 ya nyumba hizi zitajengwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, asilimia 20 katika mkoa wa Dodoma na asilimia 30 zitajengwa katika mikoa mingine.

Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.

Related Posts