Moshi. Wakati Mchungaji Kantate Munis (42) akizikwa katika usharika wa Kisamo Old Moshi, Wilaya ya Moshi, Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo amewataka waombolezaji kutumia tukio hilo kama fundisho la kuwa karibu zaidi na Mungu na kutambua katika maisha zipo dhoruba za ghafla ambazo wanadamu hawawezi kuzidhibiti.
Akitoa neno la faraja, wakati wa ibada ya Maziko ya Mchungaji Kantate, Askofu Shoo ambaye ni mkuu mstaafu wa KKKT, amesema tukio hilo pia linapaswa kuwakumbusha watu kuondokana na dhana kuwa watu wa Mungu hawawezi kukutana na dhoruba za ghafla, changamoto au matatizo.
Mchungaji Kantate ambaye alikuwa mchungaji kiongozi wa usharika wa Kimashuku, pamoja na Mzee wa usharika wa Kanisa hilo, Laban Kweka(50) walifariki dunia kwa ajali Agosti 4, 2024 baada ya gari walilokuwa wakisafiria wakitokea kwenye uimbaji wa Kanda usharika wa Gezaulole wilayani Hai, kugongwa na basi.
Wakati mwili wa mchungaji huyo ukiagwa kanisani hapo vilio na simanzi vilitawala kwa mamia ya waombolezaji waliofika kushiriki ibada ya maziko, huku wengine wakishindwa kujizuia kulia na wengine wakianguka kutokana na kuishiwa nguvu.
Katika ibada hiyo ambayo imehudhuriwa na wachungaji zaidi ya 100 kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo Dayosisi ya kaskazini alikokuwa akihudumu Mchungaji Kantate na Dodoma alikoanzia huduma, pia walihudhuria viongozi mbalimbali wa taasisi za kanisa hilo na Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Hai, Amir Mkalipa, Mbunge wa Hai, Saashisha Mafue na Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo.
Askofu Shoo amesema tukio la ajali lililosababisha kifo cha Mchungaji na mzee wa kanisa, linaweza kuwaingiza watu katika majaribu ya kumuuliza Mungu kama alikuwepo au kwa nini aliruhusu hilo litokee na kuwataka kutambua ni dhoruba ya ghafla ambayo inawafundisha kila mmoja kuwa karibu zaidi na Mungu.
“Tukio hili linatukumbusha ndugu zangu kuondokana na dhana isiyo sahihi kwamba kwa kuwa mimi ni Mkristo mwaminifu, mtumishi wa Mungu, niko ndani ya Kristo siwezi kukumbana na dhoruba ya ghafla, changamoto wala matatizo,”amesema.
Akitoa salamu za Serikali, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Amir Mkalipa amesema dereva aliyesababisha ajali anashikiliwa na polisi na kwamba uchunguzi umekamilika na atafikishwa mahakamani Jumatatu Agosti 12, 2024.
Mkalipa amesema dereva huyo aliyapita magari saba yaliyokuwa yamesimama kumruhusu mchungaji kuingia kulia katika usharika wake wa Kimashuku.
“Serikali tulichukua hatua, tunajua haziwezi kusaidia kurudisha maisha ya Mchungaji lakini tayari tumechukua hatua, tumemshikilia dereva. Tumekamilisha uchunguzi na Jumatatu atakwenda mahakamani, kwa niaba ya Serikali tumechukua hatua zote za dhati na tutahakikisha ile haki ya kidunia inatendeka”
Akisoma historia ya marehemu, Naibu Katibu Mkuu Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT, Munguatosha Makyao amesema Mchungaji Kantate amebarikiwa kuwa mchungaji Desemba 16, 2007 na amehudumu katika Dayosisi ya Dodoma, Ziwa Tanganyika na Kaskazini.
Amesema Agosti 4, mchungaji Kantate aliingiza ibada katika usharika wake wa Kimashuku na baada ya kumaliza alielekea usharika wa Gezaulole kuungana na kwaya ya usharika wake kushiriki uimbaji wa Kanda na Kwaya yake ilichaguliwa kuiwakilisha kanda ya kusini katika uimbaji wa jimbo.
“Baada ya uimbaji kumalizika walianza safari kurudi Kimashuku na ndipo basi hilo lilipoyapita magari mengine na kumgonga ambapo alifariki na mzee wa Kanisa lakini Mungu aliwalinda watoto wawili yatima waliokuwa nao” amesema Makyao.
Akitoa wasifu wake, Makyao amesema Mchungaji Kantate alikuwa mchungaji mpole, mtiifu, mwenye bidii katika huduma na alikuwa mchungaji anayeheshimu taratibu na kuzifuata.
“Mchungaji Kantate pia alijawa na upendo kwa wote na alipenda kulea na kutunza vikundi hasa vya watoto. Alipenda sana kuimba na kufanya kazi za mikono kama kilimo na ufugaji na alipendwa sana na watu wengi kutokana na utumishi wake uliotukuka”.
Mchungaji Kantate ameacha mume na watoto wanne, wawili wa kiume na wawili wa kike.
Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.