Misenyi. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amemkaribisha Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu kujiunga na chama hicho akidai tayari chama chake kimeacha misingi yake.
Makalla ameeleza hayo Agosti 9, 2024 kwenye mkutano wa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi uliofanyika katika Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera anakoendelea na ziara ya siku nne.
Ukaribisho huo umetolewa zikiwa zimepita siku chache baada ya Lissu kunukuliwa akisema Chadema si mama yake na kwamba, atakuwa tayari kukihama chama hicho endapo kitakiuka misingi yake.
Hata hivyo, alipotafutwa Lissu amesema, “Mimi nijiunge na chama chao? Yaani niende CCM kwa sababu gani au wana misingi ipi?CCM kuna nini niende kufuata? Tukajenge Taifa kwa… muulizeni Makalla anafikiria mimi nitajiunga na CCM?,’’ amehoji.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Makalla amemkaribisha Lissu kujiunga na CCM akidai tayari chama chake kimepoteza misingi yake, hivyo anakaribishwa kujiunga na CCM ili wafanye kazi pamoja kulijenga Taifa.
Amedai kwa sasa Chadema ni chama kisichofuata misingi ya demokrasia, kinakabiliwa na rushwa, viongozi wake hawana mpango wa kutoka madarakani na hakihubiri umoja wa kitaifa, hivyo Lissu hana sababu ya kuendelea kuwa huko.
“Kwa usomi wake Tundu Lissu, sehemu pekee ya kufanya siasa ni kwenye Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo nimkaribishe ndugu yangu Lissu aje tufanye kazi, tuijenge nchi yetu,” amesema Makalla.
Awali, akizungumza kwenye mkutano huo, Mchungaji Peter Msigwa, aliyehama kutoka Chadema na kujiunga na CCM, amemweleza Lissu kwamba tayari chama chake kilishakiuka misingi yake.
“Nimemsikia Lissu akisema Chadema si mama yake, atakuwa tayari kukihama chama hicho endapo kitakiuka misingi. Nimwambie ndugu yangu Lissu kwamba Chadema kilishakiuka misingi yake, hamna kitu tena pale,” amesema Mchungaji Msigwa aliyewahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini kupitia Chadema.
Amesema hakutaka kuwa mnafiki, ndiyo maana aliamua kukihama chama hicho ili aendeleze kazi ya kuwatumikia Watanzania kwa kuwa alibaini Chadema hakikuwa na misingi imara ya uongozi.
Wakati huohuo, mbunge wa Nkenge (CCM), Florent Kyombo amesema wananchi jimboni humo wanakabiliwa na changamoto ya vitambulisho vya Taifa, huku akieleza Jeshi la Uhamiaji linawanyanyasa wananchi wanapotafuta vitambulisho hivyo.
“Tunaomba Jeshi la Uhamiaji lihudumie watu kwa weledi, watu wetu wanapata manyanyaso kutoka kwa askari wa Uhamiaji. Tunataka watu wenye sifa wapewe vitambulisho vyao bila kusumbuliwa,” amesema mbunge huyo.
Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Rabia Abdallah Himid, amewahamasisha wananchi kwenda kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapigakura, ili wapate fursa ya kuwachagua viongozi kwenye chaguzi zijazo.