Mwanza. Baadhi ya vyama vya siasa mkoani Mwanza, vimeiomba Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuangalia uwezekano wa kugharamia posho kwa ajili ya mawakala wa vyama hivyo, wakati wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Wakizungumza leo Ijumaa Agosti 9, 2024 kwenye mkutano wa wadau wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa daftari hilo mkoani Mwanza, wamesema kwa kufanya hivyo kutatoa uwanja sawa kwa vyama vyote vya siasa kuwa na uwakilishi wakati wa uboreshaji wa daftari hilo, kwa kuwa si vyote vina uwezo wa kugharamia mawakala.
Mwenyekiti wa chama cha National Reconstruction Alliance (NRA) Mkoa wa Mwanza, Ahmad Mkangwa amesema baadhi ya vyama hivyo havina uwezo wa kuwagharamia mawakala wake, hivyo kupoteza haki ya kuwepo kwenye vituo vya uandikishaji.
“Kama unavyojua uwezo wa vyama unatofautiana, tusije kuingia peku wengine wamevaa viatu … tutaachwa,” amesema
Akijibu ombi hilo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima amesema tume haitotoa posho kwa mawakala kwakuwa sio jukumu lake lililobainishwa kisheria na kuvisisitiza vyama hivyo kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kuboresha taarifa zao ili kuwa na kigezo cha kuwachagua viongozi wanaowataka.
Naye, Sophia Donald kutoka shirika lisilo la kiserikali la Sauti ya Wanawake ameiomba tume iangalie vigezo vya maeneo na shughuli wanazofanya watu wakati wa kupanga tarehe za kuboresha taarifa zao, akidai ana wasiwasi wa siku saba za uandikishaji mkoani Mwanza ni chache hasa visiwani ambapo wavuvi hawakai kambi moja bali kulingana na mzunguko wa mazao ya samaki.
“Lakini pia Kisiwa cha Ukerewe kina visiwa vidogo vidogo zaidi ya 30 kati ya hivyo 15 vina makazi … kutoka kisiwa kimoja kwenda kingine ni zaidi ya saa saba, na wasiwasi kama siku hizo watu wote watapata fursa ya kuboresha taarifa zao,” amesema.
Hata hivyo, Kailima amewaondoa wasiwasi akidai siku saba zinatosha wakazi wa mkoa huo kuboresha taarifa zao akiwataka kuacha tabia ya kujitokeza kwenye uboreshaji siku ya mwisho badala yake waanze kujitokeza siku ya kwanza.
“Mfano Katoro (Geita) tuliongeza mashine tano baada ya kuona idadi kubwa ya watu waliojitokeza kujiandikisha … siku saba zinatosha, kwa utamaduni wetu hata ukiweka mwezi mzima watu watakuja siku ya mwisho,” amesema
Awali akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele amesema mzunguko wa tatu wa uboreshaji wa daftari hilo utajumuisha mikoa ya Mwanza na Shinyanga ambapo utaanza Agosti 21 hadi 27, 2024.
“Vituo vitafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni. Mkoa wa Mwanza kuna vituo 2,251 vitakavyotumika kwenye uboreshaji kwa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 73 katika vituo 2,178 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.