Dar es Salaam. Mawakala wa meli Tanzania wametaja kero tatu zinazowatatiza katika shughuli zao ikiwemo gharama kubwa ya usafirishaji wa mizigo kwa njia ya barabara.
Changamoto nyingine ni utozaji wa kodi kwenye meli kabla ya kutia nanga tofauti na utaratibu wa kimataifa unaoelekeza meli itozwe kodi baada ya kufunga kitendo ambacho kwao kinawatengenezea hasara.
Kero ya mwisho ni mabadiliko ya kanuni mara kwa mara ya kodi bila wao kushirikishwa, jambo ambalo linaathiri uwekezaji wao.
Hayo yameelezwa leo Agosti 9, 2024 na wawakilishi wa Kampuni ya Uwakala wa Meli Tanzania Sturrock Flex Shipping na kampuni ya Nyota katika ziara ya Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile.
Kihenzile amefanya ziara kwenye kampuni hizo zinazodhibitiwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazotatiza taasisi zilizowekeza kwenye sekta ya uchukuzi kwa ajili ya kupata ufumbuzi.
Akiwasilisha kero hizo, Meneja wa Fedha Kampuni ya Nyota Jimmy Kabwelle amesema mabadiliko ya mara kwa mara ya sera za Serikali yanawaathiri kwenye uwekezaji.
“Sera za Serikali zinabadilika mara kwa mara, mwaka 2019 tulikuwa na ada kwenye meli lakini iliondolewa kupitia tamko. Pia tatizo lingine ni gharama za usafiri mizigo kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam ni ghali kuliko kusafirisha mizigo nje ya nchi,” amesema.
Katika usafirishaji wa mizigo kwa njia ya meli, Kabwelle amesema mwaka 2023 asilimia 60 ya mizigo ya madini ya shaba kutoka DRC Congo na Zambia zilipitia nchini.
Amesema kiwango cha madini ya shaba iliyozalishwa na nchi hizo mwaka 2023 ni tani milioni 3.4 na zilizopita bandari ya Dar es Salaam ni tani milioni 2.1.
Kwa upande wa Kampuni ya Sturrock, Meneja Mkuu Hashim Ahmed amesema suala la utozaji wa kodi ya kuhudumia mizigo, wamekuwa wakitozwa na wamekuwa wakilalamikia bila kupata majibu.
“Pia tunalipia meli kabla ya kufunga na utaratibu wa kimataifa meli inapaswa kulipiwa baada ya kufunga, ukiangalia bandari zingine utaratibu sio huu,” amesema.
Akijibu changamoto hizo, Kihenzile amesema suala la uwepo wa kodi na baadaye kuondolewa ni changamoto ambayo Serikali inaiondoa, kwa kutengeneza mazingira ya nchi kutabirika kwenye uwekezaji.
“Changamoto hizi tumezisikia na tutazifanyia kazi, dhamira ya Serikali ni kuona sekta binafsi inafanya kazi kwa ufanisi na kufika kwangu hapa ni maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwasikiliza na kuzitafutia majibu changamoto mnazopitia,” amesema Kihenzile.
Maelekezo hayo ya Rais Samia ni yale ya Julai 29,2024 wakati akiongoza kikao cha Baraza la Taifa la Biashara TNBC, alipowaagiza wasaidizi wake wakiwamo mawaziri kukaa meza moja na sekta binafsi ili kutatua changamoto zao.
Kauli hiyo ni kutokana na malalamiko yaliyoibuliwa na sekta binafsi katika kikao hicho kilichoongozwa na Rais Samia ambaye alisema baadhi ya changamoto zilizoibuliwa hazihitaji fedha bali ni maamuzi ya watendaji wake Serikalini.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa TASAC Nelson Mlali, amesema uwekezaji wa Serikali katika ujenzi visima vya kuhifadhia mafuta Kigamboni, utasaidia kuharakisha uhudumiaji wa meli za mafuta katika bandari ya Dar es Salaam.