Siri imefichuka… Kilichoipa Yanga ushindi chaanikwa

UMELIONA lile bao la Yanga lililowapa ushindi muhimu wa bao 1-0 dhidi ya Simba? basi tambua kwamba zile ndio pasi nyingi pekee zilizopigwa mfululizo kwenye mchezo huo uliochezwa kwa dakika 71 badala ya 90.

Yanga juzi, iliifunga Simba kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa Nusu Fainali ya pili ya Ngao ya jamii iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ukiwa ni ushindi wa tatu mfululizo.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga sasa kesho Jumapili itakutana na Azam FC kwenye mchezo wa kuamua nani atakuwa bingwa mpya wa taji hilo ambalo Simba imelitema juzi.

Bao la Yanga lilipatikana dakika ya 44, likianzia kwenye eneo lao kwa mpira wa kurushwa na beki wao wa kulia Yao Atohoula Kouassi kisha wakapiga pasi 14 mpaka wanaweka mpira wavuni bila ya Simba kugusa mpira.

Wakati pasi hizo zinapigwa wachezaji saba wa Yanga wakigusa mpira alikuwa Duke Abuya aliyepiga pasi nyingi kwenye shambulizi hilo akigusa mpira mara nne tofauti akifuatiwa na wenzake Pacome Zouzoua na mfungaji wa bao Maxi Nzengeli waliotoa pasi mara tatu mpaka bao hilo linafungwa.

Wengine walioshiriki bao hilo walikuwa Boka, Yao, Aucho na Dube aliyetoa pasi ya mwisho ya bao hilo ambao kila mmoja aligusa mpira mara moja.

Nidhamu Simba ya kukaba haikuwa nzuri ambapo mpaka bao hilo linafungwa pasi hizo zikipigwa kwa sekunde 33, timu nzima ya wekundu hao ilikuwa kwenye eneo lao na ikashindwa kutegua mtego huo na kuruhusu bao kikiwa ndiyo kipindi kwenye mchezo huo ambacho zilifanikiwa kupigwa pasi nyingi zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Mchezo huo uliamuliwa ndani ya dakika 90 lakini ukachezwa kwa dakika 71 tu huku zikipotea dakika 19 zikipotea kwa matukio tofauti.

Kipindi cha kwanza kilichezwa kwa dakika 36:07:03 huku kipindi cha pili kikichezwa kwa muda mchache dakika 34:56:32 na kufanya jumla kuchezwa dakika 71.

Matukio makubwa yaliyoufanya mchezo huo kupotea muda ni makipa kupoteza muda wakati wa kuanzisha mashambulizi, wachezaji kuumia ambapo Simba ilipoteza muda zaidi kipindi cha kwanza huku Yanga ikipoteza muda kipindi cha pili.

Kipa wa Simba Mussa Camara alikuwa kinara wa kupoteza muda kipindi cha kwanza akitumia sekude 8-9 kupiga mpira anapoudaka au hata kuanzisha mashambulizi.

Mwenzake wa Yanga Djigui Diarra naye akamlipa kipindi cha pili akitumia sekunde 8-11 kuanzisha mashambulizi kwenye mchezo huo.

Kulikuwa pia na makosa kwa mwamuzi Heri Sasii kwenye mchezo huo pamoja na msaidizi wake wa kwanza Mohammed Mkono ambayo yalishindwa kutoa haki kwa timu zote mbili tena yakiwa matukio makubwa.

Matukio hayo ni kwamba timu zote mbili zilinyimwa penalti kipindi cha pili ikitangulia Yanga kwa tukio la Stephanie Aziz KI kuangushwa eneo la hatari marejeo ya picha yanaonyesha kuwa ulikuwa ni mkwaju wa penalti.

Yanga tena ikanyimwa nafasi nzuri ya kufunga bao la wazi kupitia Aziz KI akipokea pasi ya Mudathir Yahya lakini Mkono akaamua kwamba mfungaji alikuwa ameotea wakati anapokea mpira huku pia marejeo ya picha yakionyesha kuwa alikuwa sehemu sahihi.

Pia marejea ya picha yanaonyesha kuwa faulo ambayo Boka alimchezea Kijili dakika za mwisho za mchezo huo ilistahili kuwa penalti.

Mwamuzi mkongwe wa zamani Ibrahim Kidiwa ameliambia gazeti hili kuwa, timu zote zilinyimwa penalti halali huku Yanga wakinyimwa na bao.

Kidiwa alisema hataki kumlaumu sana Sasii kwa kuwa hata wao wanapata nafasi ya kuzungumzia hilo kupitia mikanda ya marudio ya video lakini timu zote zilinyongwa kwa matukio hayo matatu makubwa mchezoni.

“Ukiangalia lile tukio la penalti ya Simba, mwamuzi alikuwa karibu akilitazama pale hakuwa na haja ya kuhitaji msaada wa mwamuzi msaidizi ambaye lile tukio lilikuwa linatokea kwa nyuma yake kidogo,” alisema Kidiwa.

“Hata ile penalti ya Aziz KI nayo ni penalti ya wazi hata lile bao halikuwa na shida lakini sitaki kumlaumu sana kwa kuwa sisi tunasema haya kwa faida ya kupata mikanda ya marudio ya video.

“Bao la Aziz KI huwezi kumlaumu mwamuzi wa kati kwa kuwa anayefanya maamuzi ya kujua nani amezidi ni mwamuzi wa pembeni, pale atajibu yule mwamuzi wa kwanza msaidizi (Mohamed Mkono), ambaye ndiye aliyemsaidia mwamuzi wa kati juu ya tukio husika.

“Unajua hii taaluma yetu inatutaka kufanya maamuzi kwa asilimia mia moja kwa kile unachokiona na makosa haya ni ya kibinadamu yanatokea ila ukiyarudia kwa umakini unaiona hiyo shida kwamba yalitakiwa kuamuriwa tofauti.”

Yanga imedhihirisha kwamba bado ni tishio kwa namna ilivyoishinda mechi hiyo dhidi ya Simba, ikicheza mpira mzuri wa mbinu huku ikiwa imara pia kwenye ulinzi.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, walikuwa imara zaidi katika kuipa presha Simba inapokuwa inamiliki mpira ambapo Simba ilijikuta ikipiga pasi nyingi ikiwa kwenye eneo lao na ikipiga pasi chache kwenye eneo la wapinzani wao.

SIMBA TIMU IPO,  MUDA UTAONGEA

Kutokana na kiwango ambacho wamekionyesha dhidi ya timu iliyokamilika kama Yanga ni dhahiri kuwa Simba imefahamu inatakiwa kufanya nini na imeanza kazi hiyo vizuri.

Simba iliyosajili wachezaji 14 wapya ikiwa na benchi jipya la ufundi chini ya kocha Fadlu Davids, inahitaji muda kuweza kujipata sawasawa ambapo ilicheza hivyo ikiwa na takribani wiki tatu tu kambini.

Mashabiki wa Simba na hata viongozi wao wanatakiwa kuelewa kwamba wapo kwenye mchakato wa kupata timu bora lakini haitakuwa haraka sana kufika wanakotamani  na hilo walilionyesha juzi baada ya kuwapigia wachezaji wao makofi ya pongezi mara baada ya filimbi ya mwisho ya mchezo huo.

Kiwango alichoonyesha kipa wa Simba Camara hata Aishi Manula angekuwepo angejua kwamba amepata mpinzani sahihi kutokana na namna alivyoonyesha ubora wa kucheza krosi na hata kuokoa michomo mikali lakini uwezo wake wa kuutumia mguu ni jambo lingine ambalo linamtofautisha na makipa wengi nchini.

Ukiacha Camara kiungo Deborah Fernandez, pale Simba imepata kiungo bora mshindani ambaye anasaidia kukaba na hata kupandisha mashambulizi akiwa na ujasiri mkubwa, pia yumo winga Joshua Mutale ambaye alikuwa na kitu kwa mbio zake kuwahi lango la wapinzani.

Yanga nao wana watu wao wapya watatu walioanza nao mchezo huo ambao wameonyesha kiwango kikubwa, Duke Abuya ambaye ameingia haraka kwenye falsafa za timu hiyo akicheza kwa kiwango cha juu.

Mbali na Abuya, pia Boka  uwezo alioonyesha unadhihirisha kuwa Yanga imepata beki waliyetamani kumpata kwa kupandisha mashambulizi na hata kukaba huku pia akiwemo Dube licha ya kushindwa kufunga lakini asisti yake ilikuwa ya akili kubwa na namna alivyowapa wakati mgumu mabeki wa Simba.

Kama kuna mtu aliwasumbua Simba ndani ya dakika 90 basi alikuwa huyu Pacome, mbio zake akiwa na mpira na umiliki wake wa mpira ulikuwa wa kiwango kikubwa na kuwapa wakati mgumu wekundu hao.

Kila apokuwa na mpira wachezaji wa Simba walihitajika kuwa makini zaidi dhidi yake wakijua kwamba anaweza kufanya kitu tofauti, mara nyingi Yanga ilipokuwa chini aliirudisha mchezoni kwa nguvu, kasi na akili yake ya ubunifu.

Kocha wa Yanga Miguel Gamondi akizungumzia mchezo huo alisema haikuwa rahisi kwao kushinda huku akikiri Simba iliwapa upinzani lakini akawapongeza wachezaji wake kwa kucheza na nidhamu kubwa.

“Tulifanya kile ambacho tunafanya mazoezini, hivi ndio namna tunafanya mazoezi yetu, nawapongeza Simba, nilisema wamebadilika lakini tuliendelea kuwa bora zaidi yao.

“Tungeweza kushinda kwa mabao mengi lakini kuna mambo yalitupunguzia ushindi wetu, nadhani kama waamuzi wangekuwa katika ubora wao mambo yangekuwa tofauti sasa tunaiangalia fainali ambayo nayo itakuwa ngumu.”

Kwa upande wa Fadlu ambaye amepoteza dabi yake ya kwanza, alisema timu yake licha ya kupoteza anajivunia namna vijana wake walivyojituma kwenye mechi hiyo.

“Hii ni kama tuna wiki tatu na nusu tumecheza hivi, nawapongeza wachezaji wangu walicheza vizuri lakini nadhani kwa hiki tulichoonyesha kuna mengi mazuri tutaweza kuyafanya, nawapa pole mashabiki wetu kwa kupoteza mechi kubwa lakini nimewapenda namna walivyoiunga mkono timu yao,”alisema Fadlu.

Related Posts