Rombo. Polisi Mkoa wa Kilimanjaro wanamshikilia mwanamume mkazi wa Kijiji cha Mahango wilayani Rombo, akituhumiwa kumfanyia matendo ya ukatili, udhalilishaji na kumuua kwa kumnyonga mtoto wa miaka saba, Amedeus Laurent.
Mwili wa mtoto huyo ulifichwa kwenye shamba la migomba.
Mama mzazi wa mtoto huyo alifika kituo cha Polisi Agosti 6, 2024 kutoa taarifa kuwa mtoto wake haonekani tangu Agosti 5 saa 12.00 jioni.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa Agosti 9, 2024 imesema.
Uchunguzi uliofanyika uliwezesha kupata taarifa kuwa mtuhumiwa alionekana akiwa na mtoto huyo.
“Kutokana na taarifa hiyo mtuhumiwa alikamatwa lakini alipoulizwa alikana hakuwahi kuwa karibu na mtoto huyo,” amesema Kamanda Maigwa.
Amesema mtuhumiwa aliendelea kuhojiwa na jana Agosti 9, Polisi kwa kushirikiana na wananchi waliupata mwili wa mtoto huyo.
Amesema baada ya mtuhumiwa kufahamu kuwa mwili wa mtoto umepatikana amekiri kufanya uhalifu huo.
Kamanda Maigwa amesema Jeshi linaendelea kukamilisha taratibu zingine za kiuchunguzi ili mtuhumiwa afikishwe mahakamani.
Kamanda Maigwa ametoa onyo kali kwa wananchi wanaoendelea kujihusisha na matendo ya udhalilishaji, ukatili na mauaji kwani Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa mtu yeyote atakayejihusisha na matendo hayo na uhalifu mwingine.
Ameitaka jamii kutoa ushirikiano kuwafichua wahalifu kama hao ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Akizungumza na Mwananchi, baba mzazi wa mtoto huyo, Laurent Shayo amesema baada ya kutoka shule mwanaye alikuwa akicheza na watoto wenzake na ilipofika saa moja usiku hakuonekana, hivyo walifanya jitihada za kumtafuta bila mafanikio.
“Kesho yake Agosti 6 tulitoa taarifa polisi ya kupotelewa na mtoto, tuliendelea na jitihada za kumtafuta bila mafanikio, juzi na jana tukaamua kupiga mbiu kila mahali ndipo tukabahatika kumpata akiwa ameuawa na mwili wake ukiwa umetelekezwa kwenye shamba la migomba ukiwa umefunikwa na masago (majani ya mgomba),” amesema.
Diwani wa kata hiyo, Isack Tarimo amelaani tukio hilo la kinyama akiwataka wazazi kuhakikisha wanakaa karibu na watoto wao ili kuepuka matukio ya ukatili dhidi yao.
Amesema baada ya tukio hilo, aliwaagiza wenyeviti wa vitongoji katika kijiji hicho kupiga mbiu na kuzunguka maeneo yote ili kumtafuta mtoto huyo aliyepatikana akiwa amefariki dunia.