Serikali: Hakuna kigugumizi uanzishaji baraza la vijana

Dodoma. Kongamano la vijana la siku mbili linaanza leo Agosti 10, 2024 jijini Dodoma, huku Serikali ikisema hakuna kigugumizi cha kuanzisha Baraza la Vijana isipokuwa ushirikishwaji wa wadau ndio unaendelea ili kutengeneza chombo madhubuti kitakachoshughulika na masuala ya vijana.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amesema hayo leo Agosti 9, alipozungumzia maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana. 

Amesema wako katika hatua ya kuwashirikisha wadau juu ya jambo hilo na kuwa lazima wakubaliane kimuundo na kimifumo, litakuaje ili kuleta ufanisi.

“Pamoja na kwamba kuna nchi imeshaunda baraza hilo lakini ni lazima uangalie kuwa baraza litakuja kujibu na kutatua changamoto. Lisiishie kuwa ni baraza tu lakini mwisho wa siku halijibu. Katika kuangalia mifumo yake, ushirikishwaji wa wadau ni muhimu,” amesema.

Amesema mapendekezo ya baadhi ya taasisi yapo ambayo yanaendelea kuchakatwa.

“Kusema ni lini (litaanzishwa) itakuwa vigumu, kama tumefanikiwa la Sera ya Maendeleo ya Vijana ambalo ndilo linatengeneza ramani, hatuwezi kushindwa hicho kitu kidogo cha kutengeneza Baraza la Vijana ambalo ni jambo muhimu,” amesema.

Amesema maadhimisho yatafanyika Agosti 12, yakitanguliwa na kongamano la vijana la siku mbili jijini Dodoma linaloanza Agosti 10 likilenga kuwapa fursa vijana kutoa mawazo, maoni na mapendekezo yanayohusiana na uchumi.

Amesema kaulimbiu ya kidunia ni vijana na matumizi ya fursa za kidijitali kwa maendeleo endelevu.

Katambi amesema kutakuwa na mada kadhaa zikiwemo kuhusu Dira ya Taifa ya 2050, vijana na uchumi pamoja na masuala ya afya ya akili, ambazo zitawasaidia kueleza changamoto za ajira na jinsi ambavyo Serikali imechukua hatua kwenye maeneo mbalimbali kuitatua.

Katambi amesema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 idadi ya vijana nchini ni asilimia 34.5 na utafiti wa nguvu kazi wa mwaka 2019/2020 na 2021, unaonyesha asilimia 57 ya nguvu kazi ni vijana.

Amesema Serikali imefanya kazi kubwa katika maeneo mbalimbali, likiwemo eneo la ajira ambalo mwaka 2023/24 vijana 607,475 waliajiriwa.

Amesema kwa upande wa Serikali waliajiri vijana 430,464 na katika miradi mikubwa ya kimkakati waliajiriwa watu 204,959, huku sekta binafsi ikiajiri 359,052.

Amesema agizo lililopo ni kuwa na fomu maalumu ya kuzitaka wizara zote za kisekta kutoa taarifa za ajira katika kila mwaka wa fedha, lengo likiwa kufikia ajira milioni 1.2 kila mwaka.

Mbunge wa Viti Maalumu, Nusrat Hanje amesema baraza la vijana ni jukwaa muhimu kwa ajili ya kuwaunganisha vijana na kutafuta suluhu za matatizo na changamoto zao kwa pamoja.

Related Posts