Polisi yawaachia ‘Boni Yai’ na Malisa, watoa msimamo

Dar es Salaam. Aliyewahi kuwa Meya wa Ubungo, Jacob Boniface, maarufu Boni Yai pamoja na Mwanaharakati, Godlisen Malisa wameachiwa kwa dhamana na Jeshi la Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es salaam baada ya kushikiliwa kwa siku tatu kwa tuhuma za uchochezi.

Tuhuma za uchochezi zinazowakabili wawili hao ni kuchapisha taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Jeshi la Polisi linaua raia wakihusisha kifo cha Robert Mushi, maarufu babu G.

Tuhuma hizo zilikanushwa na Jeshi la Polisi na kudai taarifa hizo zinachochea chuki kati ya jamii dhidi ya taasisi hiyo na kwamba Mushi alifariki dunia kutokana na ajali ya barabarani. mwili wake tayari umezikwa Alhamisi nyumbani kwako, Shirimatunda huko Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro.

Kufuatia taarifa hizo Jeshi la Polisi liliwaita wawili hao kuwahoji na Aprili 25, 2024 wakaripoti kituo cha Polisi Oysterbay lakini Mkuu wa upelelezi mkoa wa Kipolisi Kinondoni akawapeleka Ofisi za Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Hata hivyo, baada ya kuripoti walishikiliwa kwa ajili ya mahojiano mpaka walipoachiliwa mchana wa leo.

Wakizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuachiwa leo Jumamosi, Aprili 27, 2024, wawili hao wamesema hawataacha kutetea haki za raia.

Jacob amesema wamepewa dhamana na watatakiwa kurudi Jumatatu asubuhi Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam.

Meya huyo wa zamani wa Kinondoni na baadaye Ubungo kupitia Chadema, amewashukuru Watanzania kwa kuwapigania hadi kuachiwa baada ya kushikiliwa kinyume cha sheria.
Licha ya yaliyotokea, Jacob amesema hataacha kupigania uhai wa Watanzania na hawapo tayari kuona watu wanapotea.

“Nimehojiwa na katika mahojiano yangu nimetaja watu waliopotea kwa majina, badala ya Jeshi la Polisi kutuona maadui watuone marafiki kuhakikisha watu hawapotei na waliopotea wanapatikana ndugu zao wazike miili, kuliko familia kukaa miezi sita mwaka bila kumuona mpendwa wao,” amesema.

Pamoja na kukaa rumande kwa siku tatu, Jacob amesema hawatanyamazishwa kwa kunyimwa dhamana akiwataka wote waliopoteza ndugu zao wapeleke taarifa kwake.

Amesema mazungumzo yao na Polisi kwa siku tatu walikuwa wakiwaeleza wao si wahalifu kwa sababu walitetea haki ya kuishi na kila mtu ana haki ya kuishi.

Kwa upande wake, Malisa amesema Jeshi la Polisi halipaswi kushughulikia watu wanaotetea kuishi kwa sababu ni haki ya kikatiba.

Jambo lingine alilosema Malisa tuhuma za kuzua taharuki kwa sababu ya kutoa taarifa ya mtu aliyepotea na baadaye kupoteza maisha hayana msingi kikatiba.
Kwa mantiki hiyo amesema hawajasababisha taharuki badala yake chanzo cha taharuki ni muuaji wa Mushi.
“Taarifa ya Polisi ilieleza Mushi aligongwa na gari Buguruni Dar es Salaam na aliyemgonga kukimbia, hivyo aliyemgonga kasababisha taharuki na pili Jeshi la Polisi mifumo yake ya uendeshaji imechangia taharuki kwa sababu gani, mwili wa Mushi ulikuwa Hospitali ya Polisi Kilwa Road taarifa ambayo ilielezwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Jumanne Muliro,” amesema.
Malisa amesema katika taarifa ya Kamanda Muliro, mwili wa Mushi ulikuwepo tangu Aprili 11 hospitalini hapo baada ya kugongwa akisisitiza wakati huo ndugu wa marehemu walikuwa wakimtafuta mpendwa wao wakishirikiana na Jeshi hilo.
“Kama ni taharuki imechangiwa na Jeshi kwani kungekuwa na mpangilio mzuri ingefahamika mwili ulikuwepo hospitalini ungetambulika mapema siku moja baada ya kifo,” amesema.

Amehitimisha kwa kusema watoa taarifa ni watu wenye nia njema na nchi, jamii na kulisaidia Jeshi la Polisi likiwatumia vyema inaweza kufanya nao kazi vizuri bila kuingia kwenye msuguano wala mgogoro.

Mapema leo asubuhi, Kamanda Muliro alisema dhamana ya watuhumiwa hao ipo wazi.

 

Related Posts