Shahidi upande wa mashtaka kesi ya kujeruhi apata kigugumizi mahakamani

 

SHAHIDI Kiran Ratilal wa upande wa mashtaka, amepata kigugumizi kwa kushindwa kueleza mahakama nani aliyetoa rufaa ya yeye kwenda kutibwa katika Hospitali ya Regency kutoka Hospitali ya Mnanzi Mmoja, Dar es Salaam huku akijua katika hospitali hiyo mume wake ndiye Mkurugenzi Mtendaji. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kiran jana alikuwa akijibu maswali ya dodoso mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Aaron Lyamuya wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika kesi ya kujeruhi na kutoa lugha ya matusi inayomkabili wanandoa Bharat Nathwan (57) na Sangita Bharat (54), ambapo yeye ndiye mtendewa katika kesi hiyo.

Wakili wa utetezi, Edward Chuwa alimtaka Kiran aeleze mahakama kwamba kwa nini alikuka kile alichoambiwa polisi baada ya kuchukua Pf3 kwamba akatibiwa katika Hospitali ya Serikali, lakini yeye aliamua kwenda Regency na pia ni daktari gani aliyetoa rufaa hiyo.

Kiran alisusa kujibu swali hilo, na kudai kuwa kwa wakati huo yeye alikuwa mgonjwa kwa hiyo hajui ni nani aliyetoa rufaa hiyo na pia hata daktari aliyemtibia hamjui, lakini alisikia sauti kuwa mwanamke.

Pia, alidai kuwa mume wake sio bosi katika Hospitali ya Regency alipokwenda kutibiwa kwa sababu kuna bodi ambayo ndiyo inashughulika na kila kitu.

Hata hivyo, Chuwa alipomtaka kutoa ripoti za hospitali alizotibiwa Mnazi Mmoja, Regency na CCBRT kuthibitisha kwamba alipata madhara katika ugomvi uliyotokea baina yake na majirani zake, alidai kuwa ripoti hizo hana, lakini zikihitajika atazileta.

Pia, Kiran alidai kuwa yeye ndiyo mwenye jukumu la kulinda usalama wa eneo ambalo mafundi wake waliweka vifaa vya ujenzi ikiwemo ndoo ya saruji ambayo yeye alidondokea humo wakati wa ugomvi.

“Shahidi kuna maelezo uliyatoa polisi, hebu ya angalie ni ya kwako na kama ni ya kwako ioneshe mahakama ni wapi kuna matusi yaliyoandikwa kwa lugha ya kihindu na kama yapo nani aliyatafsiri,” Chuwa alimuuliza shahidi

Akijibu swali hilo, Kiran alidai yeye hajui vizuri kiswahili, kwa hiyo hawezi kusoma, kwa sababu macho yake yalikuwa hayaoni vizuri kutoka na mchanganyiko wa saruji kwa hiyo askari alikuwa akimuuliza maswali yeye anajibu, hajui kilichokuwa kimeandikwa.

Shahidi huyo alijikuta kwenye wakati mgumu, baada ya kupata kigugumizi cha kueleza kama matusi yalitolewa kwa lugha ya kihindu, kwa nini kwenye hati ya mashtaka yameandikwa kwa lugha ya kiswahili ni nani aliyetafsiri.

Akiendelea kujibu maswali ya dodoso, Kiran alidai kuwa kama angetoa material ya ujenzi katika korido mshtakiwa
Sangita angeweza kushusha hali aliyokuwa nayo kabla ya mume wake kufika.

Pia, Kiran alikiri kwamba alidai kuwa akishamaliza kufanya ujenzi wa vigae ndipo atakapotoa vifaa vya ujenzi na kusafisha eneo hilo.

Nathwan pamoja na mke wake Sangita Bharat (54) wanaoishi Mtaa wa Mrima – Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam wanatuhumiwa kwa mashtaka manne likiwemo la kujeruhi waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.

Kesi imeahirishwa hadi Agosti 15,2024 kwa ajili ya upande wa utetezi kuendelea kumuuliza masawali ya dodoso shahidi.

About The Author

Related Posts