WACHEZAJI wa Namungo FC, wana matarajio makubwa kuhakikisha msimu ujao, wanapata nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa, hivyo wanajifua kupigania nafasi nne za juu.
Msimu uliopita timu hiyo ilimaliza nafasi ya sita, ila baadhi ya wachezaji wapya walioongezeka ndani ya kikosi hicho, wameongeza nguvu ni kitu kinachowaamisha kitatimiza ndoto zao.
Kiraka wa timu hiyo mkongwe Erasto Nyoni, alisema anaiona nafasi ya kushiriki michuano ya CAF kwa msimu ujao, kinachomwaminisha ni aina ya usajili uliofanywa na uongozi.
“Timu zimesajili inatoa taswira ya namna Ligi Kuu ijayo itakavyokuwa ngumu, pamoja na hayo yote, hayawezi kuondoa nia tunayotamani kushiriki michuano ya CAF,”alisema.
Kwa upande wa kipa Beno Kakolanya alisema “Hautakuwa msimu mwepesi, ila tukijituma kwa bidii, nina imani kubwa tutamaliza nafasi ambayo itatuwezesha kushiriki michuano ya kimataifa.”
Mshambuliaji Meddie Kagere, alisema wanajipanga kuhakikisha wanakuwa na msimu mzuri, kubwa zaidi wapate nafasi ya kucheza michuano ya CAF.
“Maandalizi ya msimu yana maana kubwa, yanatoa picha kwa mchezaji kile anachokwenda kukifanya katika ligi, jinsi ambavyo tunajiandaa tutakwenda kufanya makubwa,”alisema.