Siri makusanyo ya Sh2.43 trilioni,  TRA ikiweka rekodi

Dar es Salaam. Katika mwezi wa kwanza wa mwaka wa fedha 2024/2025 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Sh2.43 kiwango ambacho hakijawahi kukusanywa ndani ya mwezi mmoja.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na TRA imeeleza kuwa makusanyo hayo ni sawa na ufanisi wa asilimia 104.4 ikilinganishwa na lengo la kukusanya Sh2.24 trilioni.

“Makusanyo haya ni sawa na ukuaji wa asilimia 20.9 ikilinganishwa na Sh1.94 trilioni 1.94 zilizokusanywa katika mwezi kama huo mwaka wa fedha 2023/2024.

Ufanisi katika makusanyo na ukuaji wa makusanyo kwa mwezi Julai ni wa juu kabisa kufikiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania katika kipindi cha miaka sita iliyopita,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Kamishna wa Mamlaka hiyo, Yusuph Mwenda.

Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa ufanisi huo umechangiwa na kuboreshwa  kwa uhusiano na walipakodi kupitia njia ya mawasiliano na majadiliano baina ya viongozi wa TRA na makundi mbalimbali ya walipakodi, kufuatilia na kuchukua hatua za haraka kwenye vihatarishi vya ulipaji kodi pamoja na vitendo vya ukwepaji kodi.

Pia kuongezeka kwa usimamizi wa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania na kuendelea kuwapatia mafunzo kwa vitendo watumishi wapya, kwa lengo la kuongeza uadilifu na weledi katika utendaji kazi

Sababu nyingine ni kuongeza usimamizi wa matumizi sahihi ya mashine za EFD na matumizi ya Stempu za Ushuru wa Bidhaa (ETS).

“Ufanisi wa makusanyo uliofikiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa mwezi Julai ni kiashiria chanya katika kuhakikisha lengo la makusanyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 la Sh30.4 trilioni linafikiwa,” imeeleza taarifa hiyo.

Kupitia taarifa hiyo, TRA imeelezea kuwa imejipanga, kuimarisha uhusiano na ushirikiano na walipakodi pamoja na wananchi wote, uimarishaji utoaji wa elimu ya kodi na huduma bora kwa walipakodi wote na kujenga na kuimarisha mifumo ya kodi za ndani na forodha inayosomana na mifumo mingine.

Pia TRA imesema itasimamia na kuimarisha misingi ya mfumo mzuri wa kodi, ikiwemo haki na usawa katika utozaji kodi na kuimarisha na kusimamia weledi na huduma nzuri kwa walipakodi, ikiwemo watumishi wake kuvaa vitambulisho wanapotoa huduma ili kuweka uwazi baina ya mtoa na mpokea huduma.

Pia imesema inasikiliza na kutatua changamoto za kikodi za walipakodi kwa wakati nchi nzima na kushirikiana na tume ya Rais ya tathmini ya mfumo wa kodi nchini.

Kadhalika, mamlaka hiyo imesema itasimamia utekelezaji wa makubaliano ya Serikali na wafanyabiashara nchini ikiwemo uwepo wa kodi elekezi kwa bidhaa nane zinazoingizwa nchini, pamoja na mfumo sahihi kwa biashara za kuchangia makasha (consolidation) na kusimamia uadilifu kwa watumishi wa TRA na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria kwa wachache wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma.

Related Posts