*SIMBU NA GEAY WASHINDWA KUTAMBA MBIO ZA MARATHON ZA OLIMPIKI PARIS 2024,
TANZANIA imeshindwa vibaya kwenye mashindano ya mbio za Marathon za Olimpiki Paris 2024 baada ya tegemeo lake kuu Alphonce Simbu kumaliza nafasi ya 17 akitumia saa 2:10: 03
Geay, akiwa katika nafasi ya 74, ni mmoja wa wakimbiaji 11 ambao hawakumaliza hadi Mwisho.
Matumaini ya Tanzania kuambulia chochote sasa yamebaki kwa kinadada Jackline Juma Sakilu na Magdalena Crispin Shauri ambao kesho watatupa karata zao mwisho katika mbio za Marathon kwa Wanawake ambazo ndio zitakuwa zinahitimisha rasmi michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.
Sakilu na Shauri wataingia barabarani kuanzia saa 3 za asubuhi kwa saa za Tanzania.
Katika mchuano wa Marathon kwa wanaume leo, mshindi alikuwa Tola Tamirat wa Ethiopia akinyakua medali ya dhahabu akiweka pia rekodi mpya ya Olimpiki ya saa 2:06:26 huku nguli wa Kenya Eliud Kipchoge akishindwa kutetea taji lake, baada ya kushindwa kumaliza mbio hizo.
Tola aliingia katika mbio za marathon za Olimpiki kama mchezaji wa akiba wiki mbili zilizopita, akijaza nafasi ya mchezaji mwenzake wa Ethiopia aliyejeruhiwa.
Bashir Abdi wa Ubelgiji alimaliza wa pili na kunyakua medali ya fedha kwa kukimbia kwa muda wa saa 2:06:47, huku Mkenya Benson Kipruto akiwa wa tatu na kutwaa medali ya shaba kwa kutumia saa 2:07:00.