Unavyoweza kukabiliana na mwenza anayechepuka

Kwa nini ujichukulie sheria mkononi unapogundua na kuthibitisha mumeo au mkeo anachepuka? Kuna njia za kufanya kukabiliana na changamoto ya mweza asiyemwaminifu.

Swali hili linakuja kukiwa na mjadala kufuatia tukio la vijana watano waliombaka na kumlawiti binti mmoja kwa madai ya kupewa maelekezo ya kufanya hivyo na afande.

Kulingana na sakata hilo, afande huyo ni mke wa mwanamume anayedaiwa kuwa na uhusiano na binti huyo, hii ina maana kwamba mke aliamua kupambana na mchepuko wa mumewe kwa kumtumia kikundi cha watu kumfanyia ukatili.

Katika muktadha wa sheria, inaelezwa hakuna kesi ya mwanamke kumfumania mwanamke mwenzake, lakini ipo ya ugoni kwa wanaume dhidi ya mwanamume mwingine na kuna adhabu zake.

 Akiielezea kitaalamu sheria hiyo, Wakili Kiongozi wa Kampuni ya Uwakili ya Haki Kwanza, Alloyce Komba anasema japo wengi huwa hawaizingatii sheria ya ugoni, ipo na ikithibitika ina adhabu zake, ikiwamo ya kulipa fidia.

Hata hivyo, anasema sheria hiyo ni ya mfumo dume, hakuna kesi ya ugoni ya mwanamke dhidi ya mwanamke mwingine, bali ni kwa mwanamume dhidi ya mwanamume mwingine.

Alitolea mfano moja ya kesi alizowahi kusimamia kwenye Mahakama ya Kinondoni ambayo ilikuwa ya kuvunja ndoa na ndani ya kesi hiyo mteja wake alifungua kesi ndogo ya ugoni, ambayo alishinda na Mahakama kutaka mume alipwe fidia ya Sh20 milioni na mwanaume aliyemfumania.

“Kesi ya ugoni ina sheria yake, mradi tu uwe na ushahidi, kama nilivyosema ni sheria ya mfumo dume kutokana na mila zetu kwamba mwanamume anaweza kuoa wanawake wengi, wewe mwanamke ukimfumania akikwambia huyo uliyemkuta naye ni mke mwenzio na alikuwa tu hajakutambulisha, utamshtaki vipi?’

Hata hivyo, anasema sheria hiyo imeegemea upande mmoja wa mwanamume kumfumania mkewe na si mwanamke kumfumania mumewe na mwanamke mwingine.

“Ikitokea mwanamke kamfumania mumewe, hicho ni kigezo cha kuvunja ndoa, kuna kesi ya uzinzi na unaweza kuomba talaka kwa kuwa moja ya sababu za talaka ni mtu akikutwa anafanya uzinzi na kama bado unampenda basi unachoweza kufanya ni kumsamehe na si kuchukua sheria mkononi, hilo ni kosa la jinai,” anasema.

Kinachoendelea kwenye jamii

Deborah John (siyo jina lake halisi) wa Kimara, jijini Dar es Salaam anaeleza namna alivyovunja undugu na mdogo wake wa tumbo moja baada ya kumfumania na mumewe.

“Kilikuwa ni kipindi ambacho nimejifungua, alikuja kwa ajili ya kunisaidia, sikuwa na hofu alipokuwa na shemeji yake, wakati mwingine nawaacha wote wakiangalia TV mimi nakwenda kulala, nikijua ni mtu na shemeji yake, wakautumia huo mwanya kunisaliti,” anasimulia kwa uchungu.

Anasema siku alipowafumania hakuamini, pale ndipo ilikuwa mwisho wa ndoa yake na undugu na mdogo wake ukakoma hadi leo hawana mawasiliano.

Lushaka Peter wa Morogoro anaeleza namna alivyoingiwa na ibilisi na kuwaza kufanya kitu kibaya kwa mkewe baada ya kumfumania.

“Sijui ningefikia uamuzi niliotaka kuufanya leo ningekuwa wapi? Huwa nikiikumbuka siku hiyo naijutia sana, lakini pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa ujasiri na kustahimili.

“Siku namfumania sikuwa peke yangu, hata hivyo niliyekuwa naye alitaka tu nishuhudie uchafu wa mke wangu na alinidhibiti kwelikweli kufanya fujo, siku ilikuwa ngumu na ndoa yangu ilivunjika tukiwa na watoto wawili,” anasema.

Hiyo ni baadhi ya mifano, wapo wengine waliojichukulia sheria mkononi, wengine kufikia hatua ya kupoteza maisha ya wenza wao.

Wakili Komba anasema kumfanyia vurugu mtu aliyechepuka na mkeo au mumeo ni kosa la jinai, linaweza kukupeleka jela kama uliyemfanyia fujo ataamua kukushtaki.

“Kwa mke akikutana na kadhia hii, anapaswa kudili na mume wake na si kumfanyia vurugu mwanamke mwingine, hii ni jinai, itakupeleka jela kwa kujichukulia sheria mkononi, vivyo hivyo kwa mwanamume ambaye hatakiwi kujichukulia sheria mkononi, sheria ipo kwa mwanamume huyo dhidi ya mwanamume mwingine aliyemfumania.”

Anasema kwa mwanamke, hata ukimfumania mumeo na mwanamke mwingine unachoweza kukifanya ni kupambana na mume wako aliyevunja uaminifu na hicho ni kigezo cha kuvunja ndoa kwa kuomba talaka kwa kosa la uzinzi.

“Kama huwezi kuomba talaka basi mnarudi kule mlipooana msuluhishwe au umsamehe kama bado unampenda kwa kuwa hakuna sheria ya ugoni kwa mwanamke dhidi ya mwanamume au mwanamke mwingine,” anasema Komba.

 Viongozi wa dini wanachokishauri

 Askofu Msaidizi mstaafu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini anasema ni vema kutokuoa au kuolewa kama utaingia kwenye jambo hilo ukihitaji mwenza wako awe na tabia unazozitaka wewe.

“Mara zote huwa tunafundisha uvumilivu katika ndoa, tunafahamu ndoa ni kitu ambacho watu wawili ambao hawaelewani wanakutana, wanapendana na kuoana kila mmoja akiwa na tabia zake.

“Utofauti huo kama watachukuliana utawapa utajiri, lakini kila mmoja akitaka ndoa iwe kama anavyotaka yeye, hiyo itakuwa ni Jehanamu na itasababisha usaliti unaosababisha hadi matukio ya kikatili,” anasema Askofu Kilaini.

Anasema usaliti ni kitu kibaya, hakipaswi kufanyika na ikitokea, kama wenza wanapendana basi kikubwa ni kuombana msamaha na aliyefanya kutubu na asirudie.

“Kama mmeshindwana kabisa ni afadhali kila mmoja ashike njia yake na si kufikia hatua ya kujeruhi au kutoa uhai.

Anasema, dini haiwezi kuruhusu talaka, au kuoa wala kuolewa kwa wenza waliofikia hatua hiyo, lakini inabariki wasikae pamoja kwa sababu ndoa siyo kifo.

“Inapofikia hatua hii, ni kuwapa watoto shida bila sababu, inapaswa watu wajue ukiingia kwenye ndoa uwe umeamua kwa utulivu na ukomavu, kuchepuka kwa mmojawapo ni jambo linalosababisha chuki na hasira.

“Japo nimekutana na kesi nyingi za wanaume kuchepuka na kuzaa nje ya ndoa kuliko za wanawake ambao hawa kesi nilizokutana nazo ni za kubambikia waume zao watoto, wengi wao huwa wanasameheana na kutubu kuacha kabisa, maisha yanaendelea ingawa wanawake ndio wanasamehe zaidi kuliko wanaume.”

Anasema kwa wanaume wengi kusamehe ni ngumu, lakini kwao ni jambo rahisi kuchepuka, kikubwa ni kuziombea ndoa na familia na kusameheana ikitokea usaliti na aliyefanya asirudie, mkishindwa kabisa basi ni heri mtengane na si kuuana,” anasema.

Kwa upande wake Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhan Kitogo anasema kwa mujibu na taratibu za imani ya Kiislamu, msingi wa ndoa ni mfungamano wa hiari baina ya watu wawili wenye makubaliano ya kisheria kwa ahadi ya kuishi pamoja kwa wema na hisani na kila mmoja kumpa haki yake mwenzake.

 Anasema na ikibidi kuachana basi watu hao hawana budi kuachana kwa wema na hisani.

 “Moja ya vitu vinavyovunja ndoa nyingi ni usaliti, unaumiza na inapofikia hatua huwa tunashauri sana kuhusu uvumilivu na kutafuta suluhu.

 “Uislamu unahimiza kusameheana, katika ndoa usitake kutekelezewa haki zako kwa asilimia 100, hakuna binadamu anayeweza hilo, hivyo ili mambo yaende kila mmoja anashauriwa kujishusha kwa mwenzake, hasa hasa mwanamke.

 Anasema uvumilivu, subira na msamaha ndivyo vitu vinavyosisitizwa zaidi kwa wanandoa katika kila jambo, ikifikia wameshindwana basi waachane kwa wema na hisani na si kufikia hatua ya kufanyiana matukio ya kikatili.

 “Japo wengine huchukulia tofauti hili la kuachana kwenye Uislamu, lakini kuachana kwa wanandoa waliofikia hatua ya kutoelewana ni tiba, ndoa ni tundu la maisha, lakini kuna hatua inafikia kuna watu inawaondolea maisha yenyewe, ili wasifike huko Uislamu unasema bora watengane kwa wema na hisani,” anasema.

 Wanasaikolojia wafunguka

Wakizungumza kwa muktadha wa saikolojia, baadhi ya wanasaikolojia wanasema njia bora na rafiki unapohisi au kugundua mwenza wako anachepuka ni kuzungumza.

“Ukikaa kimya kuna namna unajitengenezea sumu mwilini ambayo isipotolewa inakwenda kuathiri mfumo wako wa neva kwa kuipa akili mzigo mkubwa, ndiyo tunaona watu wanafanya vitendo vya kikatili hadi kuua,” anasema Modester Kimonga, ambaye ni mkufunzi wa saikolojia kwenye Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Tanga.

Anasema, kisaikolojia mwanamke na mwanaume hadi kuwa wenza kuna hali ya kuvutiana kimapenzi, mnaposalitiana ile hali inakuwa imeondoka na mmoja anapokaa kimya bila kuzungumza inamsababishia athari, ikiwamo kuharibu utendaji wake wa kazi.

“Kuzungumza kama wenza ni dawa, bila kufanya hivyo mtu anatunza kitu moyoni na kutengeneza sumu inayosababisha matokeo ya haya matukio ya kikatili kwenye mahusiano ambayo nyakati hizi yanafanywa na pande zote mbili.

Anasema kama wenza wakishindwa kuzungumza na kufikia muafaka, suluhisho ni kutafuta msaada wa kisheria au wa watu wa karibu.

“Japo kijamii wanasema siyo vizuri masuala ya mapenzi kushirikisha watu wengine, lakini kuna hatua ikifika hakuna budi kutafuta msaada kama mkipambana wenyewe na kushindwa.

Mwanasaikolojia mwingine, Jacob Kilimba anasema wengi wanapogundua huwa wanapata mshtuko, hasira, huzuni na wasiwasi.

“Unapokutana na changamoto ya usaliti, kikubwa unachoweza kufanya kwa haraka ni kutengeneza usalama binafsi kwa kutojiweka kwenye mazingira ya kujiumiza kwa kitu alichofanya mtu mwingine.

“Hata kwenye usalama au ulinzi binafsi kisaikolojia tunazungumzia kuwa salama kiakili, kihisia na kitabia au matendo yako, unapaswa kufahamu aliyefanya ni mtu mwingine sio wewe na yule aliyefanya hiyo ni tabia yake, hivyo usikuingize moja kwa moja kwamba umefanyiwa usaliti.”

Anasema wengi hupata maumivu wakiona wamefanyiwa usaliti, japo wanachotakiwa ni wao kujitoa kwenye huo usaliti na kujua aliyefanya ni mwingine na aliyefanyiwa atafute utulivu wa kiakili na kihisia, ili tabia ya msaliti isimuathiri na kujiona hana thamani.

“Kwa nini ukae kwenye huzuni kwa sababu ya mtu mwingine aliyeamua kufanya usaliti? Unachopaswa ni kutengeneza utulivu wa kiakili utakaokupa muda wa kutafuta ushahidi utakaopelekea mzungumzie hilo suala kama mtakuwa peke yenu au na mtu mwingine wa tatu mkihitaji.

Anasema, baada ya mazungumzo, fanya uchambuzi wa tabia ya mwenza wako kama unaweza kuendelea naye au la.

Related Posts