BAUSI: Kina Bacca, Fei Toto wametuheshimisha

KIWANGO cha beki Abdulrahim Seif Bausi, kiliifanya Simba iishie kukitamani kwa macho, baada ya JKT Tanzania kuiwahi huduma yake, ikimtoa Uhamiaji ya Zanzibar na katika mahojiano na Mwanaspoti amezungumzia hilo.

Bausi anasema soka kwake siyo kitu cha kubahatisha, kwani baba yake mzazi Seif Bausi ni kocha wa timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, na sasa anasomea Diploma A ya CAF.

“Nimekulia katika misingi ya soka na sababu ya kuingia katika mchezo huu ni baba yangu ambaye nilikuwa namuona anafanya kazi hiyo tangu udogoni, nikajikuta naupenda,” anasema.

Anakiri kusajiliwa JKT Tanzania itakuwa mara yake ya kwanza kucheza Ligi Kuu Bara, ingawa alikuwa anaifuatilia na kuona ushindani, hivyo anajipanga kuendana nayo.

“Ligi ikianza nikicheza baadhi ya mechi, nitakuwa nimepata picha kamili, ingawa walikuwa wakicheza kina Bacca nilikuwa nawaangalia na nilikuwa nazungumza nao kupata uzoefu, ndio maana vitu vingi navielewa,” anasema.

Nje na soka, ana Diploma ya Udhibiti na Uendeshaji Bandari, (Shipping and Port Management), aliyoisomea katika chuo cha TPA, kilichopo Zanzibar.

“Sijabahatika kuifanyia kazi taaluma yangu, kwani baada ya kumaliza chuo nilipata nafasi ya kuchaguliwa timu ya Uhamiaji, hivyo nikaenda kujiunga nayo, hadi nasajiliwa JKT Tanzania natokea timu hiyo.

Anaongeza: “Baada ya kujiunga na timu hiyo, nilipata nafasi ya kupata mafunzo ya jeshini kwa muda wa miezi minane, baada ya hapo nikapata kazi ya Ofisa Uhamiaji.”

Mbali na hayo, anasema ndoto yake wakati anakua ilikuwa ni kusomea mambo ya afya kwa maana ya mfamasia (Pharmacist), lakini hakubatika kupata nafasi hiyo. ”Nilikuwa natamani kufanya kazi katika mashirika binafsi, ila nadhani haikuwa riziki aliyonipangia Mungu.” 

Ni kawaida ya binadamu kupitia matukio mbalimbali katika maisha na kwa upande wake, analisimulia la kutumbukia kisimani akiwa mdogo na asingekuwa kaka yake, huenda angepoteza maisha.

“Kuna kisima kilikuwepo nyumbani, wakati nacheza nikatumbukia humo, nilikunywa maji sana, bahati nzuri kaka yangu alitokea akaniokoa, hilo ni jambo ambalo sitakaa nilisahau kwenye maisha yangu yote,” anasema.

Tukio jingine baya ambalo alikutana nalo uwanjani, anasema msimu wa 2021/22, akiwa Uhamiaji wakicheza dhidi ya Black Sailors, alipata majeraha ya kichwa pembezoni mwa jicho.

“Ilikuwa mechi yangu ya kwanza kucheza Ligi Kuu ya Zanzibar, baada ya kuumia nilijiona kama nina mkosi, lakini nikatibiwa kisha nikaendelea na majukumu yangu,” anasema.

Anasema katika soka, pesa yake ya kwanza kuipata ilikuwa ni Sh600,000 (laki sita).

“Siwezi kutaja niliifanyia nini ama niliipata nikiwa timu gani, ila kwangu ikawa kubwa na ilinipa moyo wa kupambana zaidi kuona soka linalipa. Nikaongeza nguvu ya kujituma.”

Anasema Ligi Kuu Bara imepiga hatua zaidi, ina udhamini unaofanya thamani za wachezaji zipande kiuchumi, uwezo na kufuatiliwa ndani na nje, tofauti na Visiwani ambako maslahi ni madogo licha ya kuwepo na vipaji vikubwa.

“Maandalizi ya timu ni makubwa, viwanja vinaboreshwa, ndio maana wachezaji wengi wakitoka Zanzibar kuja Bara, wanakuwa na mafanikio makubwa kiuchumi, ukiachana na hilo wanakuwa wanajulikana zaidi na ni rahisi kupata nafasi ya kucheza kwenye nchi mbalimbali.

Anaongeza: ”Mfano msimu uliopita beki wa Yanga, Ibrahim Bacca alikuwa anatakiwa na timu mbalimbali, kutokana na promo anazozipata kwenye timu yake, yupo Feisal Salum ‘Fei Toto’ baada ya kuja Bara, timu mbalimbali zilikuwa zinamtaka.

“Ukiachana na hao, beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ baada ya kucheza Bara kapata kucheza Marekani na sasa yupo Congo, hivyo naamini nikipambana lazima nitafika mbali na hao ni baadhi tu, kuna kaka zetu waliotutangulia na wamefanya makubwa, kupitia soka la Bara.”

Anasema kabla ya kusajiliwa JKT Tanzania, Simba ilihitaji huduma yake, lakini haikuwa riziki yao, hivyo anajipanga kuhakikisha huduma yake inakuwa na mchango katika timu yake.

“Nina hamu na mafanikio, naamini nitapambana kama wenzangu ambao walionitangulia.”

Related Posts