Ishu ya Kagoma Yanga iko hivi, sababu kutocheza Simba yatajwa

MWANASHERIA wa kiungo Yusuf Kagoma, Leonard Richard, ameomba kupewa muda wa kujiandaa kujadili malalamiko yaliyowasilishwa na Yanga baada ya kesi ya kimkataba kufikishwa katika Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Wakati suala hilo likifika kwenye kamati kwa ajili ya kujadiliwa, mwanasheria huyo amebainisha kwamba Kagoma ni mali halali ya Simba kwa mujibu wa makubaliano na usajili uliofanywa na timu hiyo.

Amefunguka hayo muda mchache baada ya kumalizika kikao hicho ambapo ameweka wazi kuwa leo waliitwa kwa ajili kupitia malalamiko yaliyowasilishwa na Yanga.

Ishu hiyo imefikishwa kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji baada ya kudaiwa kiungo huyo aliyetambulishwa ndani ya Simba, pia amesaini Yanga.

“Tumeiomba kamati itupe muda ili tuweze kupitia yale yaliyowasilishwa na Yanga, tunaishukuru kamati imeridhia maombi yetu na tumeambiwa haitachukua muda hadi Agosti 20 kikao kitafanyika,” alisema na kuongeza;

“Kuhusiana na Kagoma kusaini mkataba timu zote mbili (Yanga na Simba) hili naamini wapo watu sahihi watakaotoa taarifa juu ya mkataba sahihi uliosainiwa na karatasi ya makubaliano ya awali.

“Mimi ninachokifahamu Kagoma ni mchezaji halali wa Simba, naomba nisilizungumze sana jambo hili, watu sahihi ni viongozi wa kamati ambayo tuna imani nayo itatoa majibu sahihi.”

Akizungumzia suala la mchezaji huyo kutocheza tangu amejiunga na Simba, mwanasheria huyo alisema haihusiani kabisa na masuala ya kimkataba bali chagamoto aliyonayo kiungo huyo ni kutokuwa timamu kama walivyo wachezaji wanaocheza eneo lake.

“Kagoma hayupo fiti eneo analocheza, waliopo wapo tayari japo sitakiwi kulizungumzia hili sana, kocha ndiye anatakiwa kutoa huu ufafanuzi ila uhakika ni kwamba haihusiani na suala la kimkataba kwa sababu ni mali halali ya Simba,” alisema.

Related Posts