Tabora. Wakazi wa Kitongoji cha Milembela, Uyui, Manispaa ya Tabora, wameamua kuchanga fedha kununua eneo maalumu la kuzikia baada ya awali kuzika ndugu zao katika makaburi ya Mtendeni, kutokana na kitongoji chao kukosa eneo hilo.
Akizungumza na Mwananchi leo Agosti 10, Seleman Khamis, mkazi wa Milembela, amesema kitongoji chao hakikuwa na eneo la kuzikia, hivyo walilazimika kwenda kuzika ndugu zao katika kata ya jirani, ambayo iko mbali kidogo.
“Baada ya kutokuwa na eneo la kuzikia, sisi wakazi wa kitongoji hiki tumeamua kuchangishana fedha kwa ajili ya kupata eneo la kuzikia. Ilifika wakati tukawa tunapata msiba na kulazimika kusafirisha hadi Kata ya Mtendeni, ambako tulitozwa 30,000 hadi 50,000 kwa mwili mmoja,” alisema.
Aziza Zuberi, mkazi wa Kitongoji cha Milembela, alisema changamoto ya ukosefu wa eneo la makaburi ilikuwa kubwa, lakini sasa wakazi wamejichanga na kufanikisha ununuzi wake.
“Baada ya kuteseka kwa muda mrefu, tumefanikiwa kupata eneo la kuzikia. Mwanzo tulikuwa tunalazimika kwenda umbali wa kilomita 7 hadi 10 kutoka kwetu hadi kata ya jirani, lakini sasa tumepata eneo letu ambalo tumelifanyia malipo na sasa tunaweza kushiriki mazishi ya ndugu zetu,” alisema.
Diwani wa Kata ya Uyui, Julius Nyanda, amethibitisha wakazi hao kujichangisha na kununua eneo la mazishi baada ya kuzika ndugu zao mbali na walipoishi.
“Ni kweli wakazi wa Kitongoji cha Milembela hawakuwa na eneo la pamoja la kuzikia. Waliokuwa na mashamba makubwa walizika kwenye maeneo yao, lakini wale ambao hawakuwa na eneo la kutosha walilazimika kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya mazishi,” amesema Nyanda.
“Baada ya kuona hilo, tukakubaliana na wakazi wa kitongoji hiki na tumefanikiwa kununua eka nne, ambazo sasa tumegawa. Wakristo wamepewa eka mbili na Waislamu eka mbili. Eneo lote hilo lilinunuliwa na wakazi wa kitongoji hiki kwa ajili ya mazishi ya wanaofariki,” aliongeza Nyanda bila kutaja gharama za eneo hilo.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.