KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Maxi Nzengeli amesema timu yake ina wachezaji wengi wenye ubora huku akimtaja Pacome Zouzoua na kuweka wazi kuwa kuifunga Simba kumemjenga zaidi.
Maxi alifunga bao pekee na la ushindi la Yanga wakati wakiiua Simba katika mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii na leo watarudi uwanjani kuumana na Azam katika mchezo wa fainali, huku akitamba bao dhidi ya Mnyama kwa mara nyingine baada ya zile mbili za Novemba 5 mwaka jana limemheshimisha zaidi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Maxi alisema ubora wa kikosi cha Yanga ukiachana na Zouzoua kuna Stephane Aziz Ki, Prince Dube kwanini timu isifunge mabao bora.
“Yanga ni kikosi kilichokamilika kila eneo ina wachezaji bora ambao wana uchu na mafanikio nafurahi kucheza na wachezaji wenzangu ambao wamekuwa na uchu wa mafanikio,” alisema Maxi aliyemaliza msimu wa kwanza na mabao 11 katika Ligi Kuu na kuongeza;
“Tuna kikosi ambacho kila mchezaji anatamani kucheza pamoja na sisi naamini bado tunaendelea na mapambano kujiweka vizuri zaidi, hakuna mchezaji ambaye anakubali kwamba ameiva, tunaendelea kujifunza na kuongeza ubora.”
Akizungumzia kuifunga Simba, Maxi akiwa ni mchezaji ambaye alihusika pia kwenye ushindi wa mabao 5-1 msimu ulioisha, alisema ni furaha kwa sababu inamuongezea morali ya kujiweka fiti zaidi.
“Kuifunga Simba timu ambayo ni mtani na mpinzani mkubwa wa Yanga ni kitu ambacho kinanijengea morali na sio kwangu tu ushindi huo ni kwa timu yote kwasababu msimu tunauanza vyema.”