Boka, Yanga sasa kimeeleweka Yanga

BEKI mpya wa kushoto wa Yanga, Chadrack Boka sasa kila kitu freshi Jangwani baada ya mabosi wa klabu hiyo kumalizana kabisa na FC Lupopo aliyokuwa akiichezea kwa kuwapa mamilioni ya fedha ambayo awali zilikaribia kuzuia Hati ya Uhamisho (ITC) ya mchezaji huyo aliyeanza kuwaka na kikosi hicho.

Unaambiwa, licha ya Yanga kumtangaza staa huyo wa DR Congo, lakini ilikuwa bado haijamalizia kiasi cha pesa ambacho ilikubaliana na FC Lupopo ili kumruhusu aje nchini na kuchelewesha ITC ya beki huyo.

Lakini kwa sasa taarifa zinasema tayari Yanga imeshafanya malipo kwa Lupopo sehemu ya kwanza ya Dola 100,000 na kumalizia pia mgao wa pili wa Dola 50,000 ambao utahusishwa pia timu iliyomlea.

Aidha, Yanga imeshapokea ITC ya Boka rasmi baada ya kumalizika kwa mzozo wa fedha kati ya klabu mbili FC Lupopo na klabu yake iliyomlea.

Makubaliano hayo yamefanyika katika Shirikisho la Soka Congo baada ya klabu hizo mbili kuitwa mezani na kusuluhishwa.

Hata hivyo, ni kwamba Boka hataweza kucheza mechi ya Vital’O kwa kuwa alichelewa kuwasilisha ITC yake lakini atacheza mechi ya pili kama Yanga itafuzu hatua hiyo.

“Yanga imeshamalizana na FC Lupopo na mgao wa pili umeshakwenda kwa timu iliyowahi kumlea hivyo Boka sasa yupo huru,” taarifa za ndani za kutoka Yanga zilisema.

Yanga itacheza na Vital’O ya Burundi Agosti 17 kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Related Posts