Ukistaajabu ya watoto wa 2000, jiandae kuyaona ya kizazi cha Alfa

Dar es Salaam. Ni bomu linalosubiriwa kulipuka, ndivyo inavyoelezwa kuhusu mwenendo wa vijana wa kizazi maarufu cha Gen Z, nchini Tanzania wakifahamika kwa jina la watoto wa 2000.

Hata hivyo, kihalisia kundi hili linahusisha vijana waliozaliwa kati ya mwaka 1997 hadi 2012 ambao kwa mujibu wa Ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 nchini Tanzania, wanakadirwa kuwa milioni 20.2, sawa na asilimia 31 ya Watanzania wote.

Miaka ya karibuni kundi hili la vijana limeonekana kuwa na mitazamo tofauti na utaratibu wa kuchukua maamuzi ‘magumu’ bila kuhofia chochote.

Ujasiri huo hauonekani tu kwenye maisha binafsi, bali hata katika kuleta msukumo kwenye mambo ya kitaifa kama ambavyo imeonekana kwenye mataifa kadhaa ya Afrika, ikiwemo nchi jirani ya Kenya ambako waliandamana kupinga Muswada wa Sheria ya Fedha waliodai unaongeza ugumu wa maisha, hadi Rais William Ruto akakataa kuusaini.

Hivi karibuni akiwa ziarani mkoani Morogoro, Rais Samia Suluhu Hassan alieleza hatari ya kutokuwapo kwa chakula na kupanda zaidi kwa bei ya sukari nchini, kunaweza kuwaingiza barabarani vijana wa kizazi cha Z, maarufu Gen Z.

“Wanasema chakula ni siasa, kukiwa hakuna chakula ile Generation Z haitatulia, itaingia barabarani, au ukiwapandishia sukari kilo ikauzwa kwa Sh7, 000 hawatatulia, hivyo ni jukumu la Serikali kusimamia masilahi ya makundi yote,” alisema.

Wakati wasiwasi ukibainishwa kuhusu kundi hilo, watu mbalimbali waliozungumza na Mwananchi, mbali na kukichambua kizazi hicho, wamesema jicho kali zaidi linapaswa kuelekezwa kwenye kizazi kinachofuata baada ya Gen Z, yaani  Generation Alpha.

Wamesema kinachotazamwa kwa Gen Z na kinachotazamiwa kwa Gen Alfa ni matokeo ya kukosekana mfumo bora wa malezi hali iliyosababisha kutengenezwa bomu ambalo linaweza kulipuka wakati wowote sasa au baadaye.

Akizungumzia hilo, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza amesema jamii inapaswa kujipanga na madhara ya ‘bomu’ hilo ikiwa ni matokeo ya malezo ya vijana wa kizazi hicho.

Amesema changamoto ya kizazi hicho inaanzia kwenye malezi, huku kukiwa na daraja kubwa la ufahamu na matumizi ya teknolojia kati yao na wazazi wao, hivyo kuwa mbele zaidi yao kwa kila kitu.

“Tunayoyaona katika nchi za wenzetu hata hapa yatatokea ni suala la muda, kinachochelewesha hilo ni rushwa kwa kuwa mfumo wetu wa utawala unaweza kutumia fedha kuwarubuni baadhi ya vijana wa kundi hili na wakatumika kuwatuliza wenzao.

“Hata hivyo, jitihada hizo ni za muda siyo za kudumu, bomu hili litakuja kulipuka. Tunachotakiwa kufanya ni kujipanga na madhara yake. Watawala watambue kwamba kizazi hiki hakidhibitiki kwa nguvu ya risasi, virungu wala mabomu, nguvu ipo kwenye teknolojia na ndiyo kundi hili lipo huko,” amesema.

Akiwa na mtazamo kama huo, Rebeca Gyumi, mwanaharakati wa haki za wasichana, amesema kusipokuwa na mikakati madhubuti ya kutatua changamoto za kizazi hicho, kitakuwa kama bomu linalosubiriwa kulipuka.

“Hiki ni kizazi ambacho ni rahisi kwao kutafuta suluhisho katika njia ambazo wanahisi watapata matokeo ya haraka. Ni muhimu ikawepo mikakati ya kuwekeza kwenye kundi hili na kutatua changamoto zao kwa kuwa ndiyo hawa wako vyuoni, wengine wanahangaika kutafuta ajira na mambo kama hayo.

“Kwa hali na mitazamo waliyonayo, nachelea kusema wagombea katika chaguzi zijazo wajiandae vyema kwa sababu wanaenda kukutana na kizazi kinachohoji. Hawataki kusikia habari za historia, wanachotaka ni mabadiliko, hawaogopi chochote na kwao siasa za matokeo ni kipaumbele,” anasema.

Rebeca ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative, anasema hatari iliyopo kwa kundi hilo ni kukosa elimu sahihi ya afya ya uzazi, ndiyo sababu kumekuwa na ongezeko la maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa vijana, hasa wasichana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24.

“Ukifanya tathmini kwa kina, rika hili (Gen Z) ndilo liko kwenye mitandao ya kijamii lakini bado nguvu kubwa haijaelekezwa huko kulipa elimu ya afya ya uzazi na kampeni za kupamba na Ukimwi, huenda kampeni hizo zinafanyika ila siyo kwa njia sahihi na matokeo yake elimu haifiki kwa walengwa na maambukizi mapya yanaendelea kurekodiwa kwa vijana,” amesema.

Ameeleza, “miaka ya nyuma kampeni za kupambana na Ukimwi zilishika kasi lakini sasa hivi zimepungua wakati ndiyo zinahitajika zaidi ili kuwanusuru vijana. Vijana hawa ni kundi ambalo liko hatarini zaidi kutokana na utandawazi na wazazi hawana muda wa kuwafuatilia watoto.”

Mwanasaikolojia Deo Sukambi anasema kizazi hicho kinahusisha watoto waliozaliwa wakati dunia inaingia kwenye mapinduzi ya intanenti na kukutana na wazazi ambao wanatumia muda mwingi kwenye kutafuta kuliko kulea.

Amesema matokeo ya hayo kimepatikana kizazi ambacho ni kigumu kutawalika na kinaweza kufanya dunia kuwa mahali hatari pa kuishi.

“Ni aina ya watoto ambao wamekuwa wakishuhudia wazazi wao wakigombana mbele yao, tofauti na ilivyokuwa sisi wazazi wetu waligombana chumbani na walipotoka nje hakuna aliyeonyesha kama kuna tatizo.

“Ni kizazi ambacho kimezaliwa na kukutana na kelele nyingi za redio, televisheni na mambo mengi yanayowafanya kujiweka kando na vile vitu walivyokuwa wanafanya watu wa kizazi cha milenia. Hawa wanaamini Serikali ni mfumo wa kinyanyasaji na hawana chama wala hawaamini katika siasa,” amesema na kuongeza:

“Hawa kwa kiasi kikubwa madai yao siyo halisi lakini wanaamini wanaweza kupambana na majibu yakaja, hivyo hutakiwi kushindana nao kwa kuwa ukifanya hivyo watakuumiza na ukikubaliana nao watakupoteza.

“Ni muhimu kukaa nao na kuwasikiliza, huku ukikumbuka si kizazi ambacho unaweza kukitisha au kukipiga mkwara,” anaongeza.

Kwa mujibu wa Sukambi, vijana wa kizazi hicho wana changamoto kubwa ya maadili na wengi wao hufanya mambo ambayo hapo awali yalikuwa hayaonekani kwa vijana.

“Hawajali chochote, anaweza kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtu yeyote na wakati wowote. Huko vyuoni siku hizi kuna mtindo wenyewe wanaita ‘friends with benefits’ (marafiki wa faida), yaani kijana wa kike na wa kiume wanaweza wasiwe na uhusiano wa kimapenzi lakini wakawa tayari kufanya mapenzi wakati wowote na kila mmoja akaendelea na maisha yake mengine.

“Hii imekuwa kawaida kabisa kiasi kwamba yule mwenye tabia na mawazo tofauti anaonekana wa ajabu. Imefikia hatua wale vijana ambao wamelelewa katika misingi mizuri wanakuwa na maisha magumu vyuoni na kila wanapokuwa na wenzao wa rika moja,” amesema.

Sukambi anasema tabia nyingine ya kizazi hicho ni kujiweka mbali na nyumba za ibada, jambo linalothibitishwa na mzazi mmoja aliyezungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa jina.

“Kwa kweli napata wakati mgumu mno kumshawishi kijana wangu twende kanisani, mkimpa taarifa kwamba kesho wote tunakwenda kanisani anachukia,” amesema.

Wakati ikiwa hivyo kwa kizazi hicho, Sukambi anatahadharisha hatari zaidi inakuja kwa kizazi kinachofuata baada hiki, ambacho kinafahamika kama Gen Alfa.

Anasema kizazi hicho kinahusisha watoto waliozaliwa kuanzia mwaka 2013 hadi watakaozaliwa 2025, ambao kwa kiasi kikubwa akili zao zimetekwa na ulimwengu wa kidijitali kuliko kilichotangulia.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 watoto waliozaliwa kuanzia mwaka 2013, ambao umri wao ni kuanzia miaka 9 kushuka chini walikuwa milioni 18.4, hii ni sawa na asilimia 30 ya watu wote nchini Tanzania.

Sukambi anasema kizazi hicho kitakuwa zaidi ya Gen Z, kikiwa na imani kubwa na kile wanachokipata kutoka kwenye intanenti.

“Hawa ni kama maroboti, wanahoji sana na kutaka kujua kila kitu, lakini hawaamini katika kufanya kazi. Kizazi hiki kwake kila suluhusho linapatikana kwenye intaneti na ndiyo maana anaweza kujifungia hata siku nzima peke yake akiwa na simu kutafuta kila anachokihitaji.

“Kizazi hiki kinatabiriwa kuwa na mambo ya hovyo zaidi, mfano kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja, kujiua au kuua wengine kwake kitakuwa kitu cha kawaida. Kwao fedha hazipatikani kwa kutoka jasho, bali kwa njia za mkato, anaamini atakaa na simu yake na kutengeneza fedha huko,” anasema Sukambi.

Baadhi ya mambo yanayoelezwa na mwanasaikolojia huyo tayari yameshaanza kuonekana kwenye jamii kukiwa na ongezeko la matukio ya watoto wenye umri chini ya miaka 15 kujinyonga, kufuatilia zaidi katuni na mengineyo.

Mjadala mwingine unaoteka katika maeneo mengi kwa sasa ni namna kundi hili la vijana linavyojiona kuwa bora kuliko waliowazidi umri.

Akizunguzia hilo, Salma Msangi (40), ambaye ni mzazi mkazi wa Dar es Salaam, anasema mara kadhaa ameshuhudia wanawake watu wazima wakificha umri wao halisi kwa sababu ya kuhofia kejeli na mashambulizi yanayofanywa na vijana kwa kuwaita wazee.

“Ni nadra kukuta mwanamke anafurahia kuambiwa ana umri mkubwa, hii inasababisha wengi wakwepe kutaja miaka yao. Hii inatokana na taswira mbaya ambayo imejengeka kwenye jamii kuhusu mwanamke mtu mzima, utamaduni huu unakuzwa zaidi kwenye mitandao.

“Kuna utaratibu wa ajabu umeibuka hivi sasa kwa watoto kutukana watu wazima huko mitandaoni, yaani mtu unaweka picha yako anatokea mtoto anaanza kukutukana na kukushambulia kwamba wewe ni mtu mzima, mara umri umeenda. Yaani usijipende, usiongee chochote unashambuliwa kuwa wewe mzee sasa, nashindwa kuelewa kwani uzee ni laana?” anasema Salma.

“Mimi ninachofahamu utu uzima ni baraka na hata hao wanaotukana wanapaswa kutambua kuwa safari ni moja, hata wao kuna siku watakuwa wazee, ni heri wajifunze kwa hao wanaowaona wazee kwa sababu maandalizi ya uzee yanatakiwa kufanyika ujanani,” amesema.

Akishauri namna ya kuondokana na au kupunguza athari za vizazi hivyo, Sheikh Khamis Mataka, mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), anasema ni muhimu Serikali ikaingilia kati kuja na sera ya malezi itakayodhibiti masuala mbalimbali ambayo yana madhara na yanashika kasi kwa sasa.

“Changamoto ya malezi ilianzia kwa waliozaliwa miaka ya 80 ambao ndiyo wamekuja kuwa wazazi wa hao Gen Z, tunachokishuhudia sasa ni hao waliokosa malezi na wao wamezaa, hivyo hali itakuwa mbaya zaidi kadiri tunavyosonga mbele. Kilichopo ni kwamba, watoto hawalelewi bali wanafugwa,” amesema.

“Hapa ni lazima Serikali iingilie kati, iitishe makongamano ngazi ya wilaya na mikoa kujadili malezi na maadili kisha maoni yatakayokusanywa huko yawasilishwe kwenye kongamano la kitaifa. Mchakato huu utupeleke kwenye kupata sera ya malezi itakayodhibiti mambo mbalimbali ambayo tunaona yanatuletea shida kwenye jamii yetu. Ni lazima ifike mahali Serikali iwe na maamuzi kwenye suala zima la maadili,” amesema.

Sheikh Mataka ameshauri pia Serikali kushirikiana na viongozi wa dini kutengeneza mafunzo ya malezi kwa ajili ya wazazi kwa sababu imeshathibitika kwamba wazazi wengi hawajui kulea inavyostahili.

“Wazazi wa sasa hawalei bali wanafuga, wanaishi na watoto wao kama mifugo wanachohakikisha wao wanawapatia chakula, malazi, makazi na elimu. Tunatakiwa kutoa mafunzo ya malezi kwa kuwa wazazi hawana, wanatumia muda mwingi kutafuta kipato na kusahau kabisa kulea, matokeo yake ndiyo haya,” amesema.

Mtaalamu wa malezi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Maadili Centre, Florentine Senya pia ameweka msisitizo kwenye elimu ya malezi kwa wazazi na watoto.

“Watoto wakipatiwa elimu ya malezi itawasaidia sana kujitambua na kujua aina ya malezi wanayopewa na wazazi wao hayapo sawa, kwa kufanya hivi tutawaandaa kuwa wazazi bora wa kesho,” amesema.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts