Unguja. Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (Tamwa-ZNZ) kimewataka waandishi wa habari vijana kuwa mashujaa na mabalozi wazuri wa kusaidia upatikanaji wa usawa wa kijinsia kwa maendeleo ya nchi.
Hayo yameelezwa Agosti 10, 2024 na Mkurugenzi wa chama hicho, Dk Mzuri Issa Ali alipofungua mafunzo ya siku tano ya kuendeleza waandishi wa habari vijana kuandika habari za uchambuzi juu ya wanawake na uongozi nchini.
“Bado masula ya usawa hayajapewa nafasi kubwa, lakini waandishi wa habari hususani chipukizi wana nafasi kubwa kuandika masula ya usawa na kuonyesha athari, kwa hiyo ni vyema kutumia kalamu zetu kubadilisha mitazamo,” amesema.
“Vijana wa kiume haikuwa bahati mbaya kuwachagua bali tumefanya hivyo kuwajenga kuwa mashujaa, mabalozi na wanaume wa mabadiliko katika kuhamasisha usawa wa kijinsia kwa jamii,” amesema.
Dk Mzuri amasema, “tumechagua vijana wenye taaluma mbalimbali ikiwemo uandishi wa habari, waandaaji na waongozaji wa filamu ambao tunaamini watasaidia kuelimisha jamii masuala ya usawa wa kijinsia na wanawake kushiriki katika vyombo vya maamuzi.”
Mkurugenzi huyo amesema lengo ni kuona ongezeko kubwa la ushiriki wa wanawake kugombea nafasi za uongozi kupitia mipango kazi itakayoandaliwa na vijana hao ambayo itazingatia uchambuzi wa takwimu na maazimio ya nchi. Ajenda ya dunia ni kufikia usawa asilimia 50 kwa 50.
Balozi wa habari Zanzibar, Mustafa Yussuf ameitaka jamii kuondoa dhana potofu kwa wanawake katika uongozi, badala yake kuwasimamia ili kutimiza ndoto zao.
“Tumeona idadi ya wanawake viongozi inaongezeka, na ni waaminifu katika utendaji wao hata katika jamii ukilinganisha na wanaume,” amesema Mustafa.
Tamwa-ZNZ imeandaa mafunzo kwa waandishi vijana 25 kutoka Unguja na Pemba, kati yao wanawake ni 15 na wanaume 10.
Yameandaliwa kwa kushirikiana na Shirika la NED la nchini Marekani lengo ni kuongeza hamasa kwa wanawake kupata fursa sawa.