Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud amesema ipo haja kwa Tanzania kuweka mkazo maalumu wa kuzitumia ipasavyo fursa za kiuchumi zilizopo katika nchi za Afrika Mashariki na mashirika mbalimbali ya kimataifa ili kusaidia nchi kukuza uchumi na maendeleo.
Othman amesema hayo ofisini kwake Migombani Agosti 10, 2024 alipokutana na ujumbe wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulioongozwa na Waziri wa wizara hiyo, Mahmoud Thabit Kombo, aliyekwenda kujitambulisha.
Kombo amechukua nafasi hiyo katika mabadiliko ya hivi karibuni yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema Tanzania kwa Afrika Mashariki lisiwe suala la uhusiano wa kijumuiya pekee bali iwe fursa kubwa ya kiuchumi katika kuzitumia nchi ndani ya jumuiya kwa shughuli mbalimbali za kibiashara na kiuchumi, mambo ambayo ni zaidi ya ushirikiano katika uwekezaji na biashara.
“Kuna haja kubwa ya kujengwa uelewa kwa wafanyabiashara na hata taasisi za Serikali za Tanzania Bara na Zanzibar katika kuziainisha na kuzitumia fursa za kiuchumi zilizopo katika maeneo hayo jambo litakalochangia kwenda sambamba na kasi ya kiuchumi duniani,” amesema.
Amesema hatua hiyo ni pamoja na kuwawezesha wananchi kwa kuwajengea uwezo wa kuzitambua na kuzitumia fursa hizo ili ziwe na tija katika kusaidia kupunguza changamoto ya ajira kwa wananchi wa pande mbili za Muungano.
Othman amesema hatua hiyo pia itasaidia Watanzania kumudu kwenda sambamba na kasi ya maendeleo.
Ametaja baadhi ya taasisi za kimataifa kama vile Shirika la Haki Bunifu (Wipo) lenye fursa kubwa za kiuchumi na kimaendeleo lakini Tanzania na Afrika kwa jumla inakosa uwakilishi, hivyo huzipoteza.
Amesema kuna haja kwa wizara kushajiisha makongamano yakibishara na ushirikiano yatakayowezesha Zanzibar kutumia vyema fursa za kipekee zilizopo ambazo zinaweza kuinufaisha nchi kiuchumi kupitia mikutano na makongamano hayo.
Waziri Kombo amesema watajitihadi kuyatumia maelekezo waliyopata kwa viongozi mbalimbali ambayo yatawasaidia kuleta tija kwa matumizi ya fursa zilizopo.
Amesema vita vya uchumi vilivyopo duniani hivi sasa vinashinda vya silaha na kwamba, kuna haja ya kufanya kila aina ya jitihada za pamoja kuhakikisha Taifa linasonga mbele.