MBUNGE KOKA KULETA MAGEUZI YA KUKUZA VIPAJI KWA WASANII


NA VICTOR MASANGU, KIBAHA

Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka katika kuunga mkono juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kukuza na kuibua vipaji vya wasanii wa fani mbali mbali ameweka mikakati kabambe kwa ajili ya kuanzisha kliniki maalumu ambayo itaweza kuwapa fursa vijana waweze kuonyesha vipaji walivyonavyo ili waweze kutambulika zaidi kutokana na kazi wanazozifanya.

Koka ameyasema hayo wakati wa semina elekezi ambayo imewakutanisha wasanii mbalimbali wa Halmashauri ya mji wa Kibaha kwa lengo la kuweza kukutana kwa pamoja ikiwa pamoja na kubadilishana mawazo na kupeana uwezo, ujuzi ,mahalifa na mbinu ambazo zitaweza kuwasaidia kufika mbali katika sanaa ambayo wanaifanya.

Koka alisema kwamba lengo lake kubwa ni kuona namna ya kuendelea kuwakutanisha kwa pamoja wasanii mbali mbali wa Jimbo lake na kuwaweka katika Kliniki ya pamoja ambayo itaweza kuwapa fursa ya kuonyeha uwezo na vipaji walivyonavyo.

“Nafahammu katika Jimbo langu kuna vijana wengi ambao wana vipaji vya aina mbali mbali kwa hivyo nitashirikiana bega kwa bega na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha katika kuanzisha Kliniki maalumu ambayo itaweza kuwapa fursa zaidi vijana kuweza kuonyesha uwezo ambao walionao na kikubwa zaidi lengo ni kuweza kuwafanya vijana wetu waweze kufika mbali zaidi,”alisema Koka.

Kadhalika Koka aliongeza kwamba mbali na kuanzisha Kliniki hiyo maalumu ya kukuza vipaji hivyo vya wasanii amewaahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha kwa kuwasaidia baadhi ya vifaa mbali mbali ambayo vitaweza kuwasaidia kuwa na studio yao ya kisasa ambayo itakuwa ni mkombozi katika kufanya kazi zao mbali mbali za mziki

Kwa wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Simon amesema kwamba lengo lake kubwa ni kushirikiana bega kwa bega na wasanii wa Wilaya ya Kibaha kuwatengenezea mfumo mzuri ambao utawasaidia katika kuwatangaza zaidi ikiwa pamoja na kwenda nao katika vituo mbali mbali kwa ajili ya kuweza kufanya mahojiano.
Naye Mwenyekiti wa wasanii waigizaji Wilaya Jumanne Kambi amempongeza kwa dhati Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka kwa maamuzi yake ya kuweza kuanzisha Kliniki hiyo ya wasanii ambayo itawasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza vipaji vyao.


Related Posts