Kampuni ya Sukari ya Kilombero imeshiriki katika Tamasha la mwaka huu la Nane Nane, lililofanyika kuanzia Agosti 1 hadi 8 katika mikoa ya Dodoma na Morogoro.
Siku ya Nane nane ni fursa kwa Kampuni hiyo kutoa elimu na kushirikiana na wakulima kwa kuonesha manufaa ya upanuzi wa kiwanda cha K4.
Nane Nane hutumika kama kitovu cha wakulima na umma katika kuangazia maendeleo katika kilimo. Ushiriki wa Kampuni ya Sukari ya Kilombero unaonesha kujitolea kwake kusaidia na kuinua jamii ya wakulima nchini Tanzania.
Upanuzi wa kiwanda cha K4 ambao unatazamiwa kukamilika ifikapo Juni 2025, utaongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa uzalishaji wa Sukari.
Mradi huu unalenga kukidhi ongezeko la mahitaji ya Sukari huku ukitengeneza fursa nyingi kwa wakulima wa ndani. Kiwanda cha K4 kitaiwezesha Kampuni ya Sukari ya Kilombero kupata miwa zaidi kutoka kwa wakulima, hivyo kuongeza kipato chao na kuchangia maendeleo ya kiuchumi ya kikanda.
Akizungumza katika mahojiano na wanahabari mjini Dodoma jana, Meneja Mawasiliano na Mahusiano ya Wadau wa Kampuni ya Sukari ya Kilombero, Bw. Victor Byemelwa, alisisitiza umuhimu wa mpango huo.
“Tamasha la Nane Nane ni jukwaa muhimu kwetu kwani ni fursa kwetu kuungana na wakulima na kujua changamoto mbalimbali.
Muhimu kwetu ni kuendelea kutoa msisitizo kwa wakulima kuhusu kuchangamkia fursa zitakazotokana na panuzi wa kiwanda cha K4 na tupo hapa kuhakikisha wakulima wanaelewa fursa zilizopo na jinsi wanavyoweza kufaidika na mradi huu”.
Katika tamasha hilo, Kampuni ya Sukari ya Kilombero pia ilitoa vipindi vya elimu kuhusu mbinu bora katika kilimo cha miwa ili kuongeza tija na uendelevu.